Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Samia Suluhu Hassan amenadi sera na ahadi za CCM ambazo zinakwenda kuwagusa moja kwa moja maelfu ya wananchi wanaojishugulisha na shughuli za kilimo na ufugaji wilayani Igunga mkoani Tabora, leo tarehe 10 Septemba 2025.
Rais Dkt. Samia amesema kama iwapo wananchi wataichagua CCM na kumpa ridhaa ya kuongoza kwa miaka 5 mingine, serikali itajikita katika kuhakikisha upatikanaji wa matrekta ya mikopo 100 nchi nzima kwa wakulima.
Pia, serikali ya CCM itaendelea kuboresha mazingira rafiki kwa wafugaji kwa kujenga majosho na uchimbaji wa mabwawa kwa mifugo pamoja na kutoa ruzuku ya chanjo na kuwasaidia wafugaji kupata leseni za utambulisho ili kukuza biashara za wafugaji.
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema serikali ya CCM itakwenda kujenga stendi mpya ya kisasa katika wilaya ya Igunga ili kukidhi mahitaji ya mabasi makubwa kutoka mikoani.
Vilevile, Serikali itajenga Soko Kuu la Igunga ambalo litasaidia kufungua na kupanua wigo wa biashara kwa wajasiriamali.
Katika kueleza mambo mengine makubwa yatakayotekelezwa katika miaka 5 ijayo, Rais Dkt. Samia amesema serikali inatekeleza ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme kitakachojengwa ndani ya Igunga.