Air Tanzania kuanza safari za Pemba

HomeKitaifa

Air Tanzania kuanza safari za Pemba

Kwa muda sasa, ndege za ATCL zimekuwa zikisafirisha abiria na mizigo kwenda Unguja, Zanzibar na siyo Pemba, jambo linaweza kuwa linaikosesha fursa ya kufaidika na mapato katika kisiwa hicho.

Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) linatarajia kuanzisha safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda katika kisiwa cha Pemba, Zanzibar, ikiwa ni hatua ya kuongeza ushindani katika sekta ya anga nchini na kuongeza wigo wa biashara ya kimataifa.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema ndege za ATCL zitaanza kusafirisha abiria na mizigo kutoka Dar es Salaam hadi Pemba mwaka wa fedha wa 2023/24.

“Shirika letu la ATCL litaanza safari zake mwaka wa fedha wa 2023/24,” amesema Mwakibete leo Mei 16, 2022 wakati akijibu swali la Mbunge wa Shaurimoyo, Ally Juma Mohammed aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuanzisha safari za ndege kuelekea Pemba.

Katika swali lake, Mohammed amesema kwa sasa katika kisiwa cha Pemba kuna ongezeko la watu wanaohitaji usafiri wa ndege, hivyo ni muhimu wakafikiwa.

Kuanza kwa safari za ndege Pemba kutarahisisha safari za abiria na kuongeza wigo wa biashara kati ya Zanzibar na Tanzania ikizingatiwa kuwa kisiwa hicho kinasifika kwa uzalishaji wa viungo na kina vivutio mbalimbali vya utalii zikiwemo fukwe kwa ajili ya watalii.

Tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani mwaka 2021, amekuwa akilifanyia mabadiliko makubwa shirika la ATCL ikiwemo kulipunguzia mzigo wa madeni, kuliwezesha kujiendesha kibiashara ikiwemo kuongeza safari za ndani na nje ya nchi ili kufaidika na fursa za kibiashara za sekta ya anga. 

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mwakibete, mwaka 2016 kabla ya Serikali kuanza utekelezaji wa mpango wa kuifufua ATCL, shirika hilo lilikuwa linadaiwa Sh141.7 bilioni za watoa huduma mbalimbali wa ndani na nje.

Hadi Aprili 2022, Serikali imelipa madeni Sh127.1 bilioni kati ya madeni hayo.

error: Content is protected !!