Nyota kutoka nchini Tanzania , Ali Kiba amewasili Kenya kwa ajili ya tamasha lake la ‘Only One King’ litakalofanyika Naivasha na kuzungumza na waandishi wa habari na kusema kwamba Harmonize siyo rafiki yake wa karibu, baada ya kuulizwa analipi lakuongea juu ya yale aliyoyasema kuhusu lebo yake ya zamani.
“Siyo rafiki yangu wa karibu, wala hata sio rafiki yangu. Harmonize nishakutana nae mara moja tu, sidhani kama nishawahi kuzungumza nae. Lakini vilevile nisingependa kumzungumzia kwa sababu hatuna mazoea, ila ni msanii mwenzangu na Mtanzania ambaye anawakilisha vizuri tu,” alisema Kiba.
Pia, baada ya kuulizwa endapo atafungua na yeye kampuni ya michezo ya kubashiri (betting) kama msanii Diamond Platnumz aliyefungua yake hivi karibu na kuipa jina la ‘Wasafi Bet’, Kiba alijibu kwa kusema dini yake hairuhusu hivyo hajui dini ya Diamond kama pia inaruhusu au hairuhusu.
“Kwa bahati mbaya dini yangu hairuhusu, sasa sijajua dini ya Diamond,” alijibu Kiba.
Ali Kiba atasindikizwa na wasanii kama Willy Paul, Otilie Brown, Femi One, Arrow Boy na Nyashinski siku ya Jumamosi tarehe 11, 2021.