Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dkt Benson Bagonza ametoa maoni kuhusu mchango wa dini katika ujenzi wa Taifa la haki na la kidemokrasia.
Akizungumza na tovuti ya The Chanzo Initiative, Askofu Bagonza alichambua mambo mbalimbali na kueleza kwamba viongozi wa dini hawajafanya vya kutosha katika ujenzi wa taifa la haki na demokrasia.
“Hakuna dini ya Serikali, lakini hao wananchi wenye dini ndio wanaounda Serikali. Wananchi ndio viongozi wa Serikali, kwa hiyo mchango upo. Mchango wa moja kwa moja ambao kwamba wanannchi wenye dini wanaongonzwa na dini katika maisha yao ndio wanaoliongoza taifa na wanaongozwa na taifa. Kwa hiyo huwezi kuitenga dini na taifa.” amesema Askofu Bagonza.
Aliongeza, “Dini ina mchango mkubw sana katija kuzungumzia masuala ya haki kwa sababu haki kabla haijawa suala la kisheria, haki ni suala la kiroho. Kwa hiyo kwa mara nyingine tena, dini na viongozi wa dini wana nafasi kubwa sana katika kujenga taifa linaloheshimu haki, linaloheshimu utu, na linalojali kwamba demokrasia iwepo kwa sababu huwezi kuongoza wanadamu kama unavyoongoza wanyama.”
Alipoulizwa kuhusu tathmini yake juu ya mchango wa viongozi wa dini katika kusimamia ujenzi wa taifa la haki hapa Tanzania, Askofu Bagonza amesema viongozi wa dini hawajafanya vya kutosha.
Alisema ili mchango wa viongozi wa dini uonekane, ni lazima wafanye mambo matatu ambayo ni kuhubiri masuala ya haki katika mafundisho yao, kuchukua hatua wanapoona haki inapotoshwa na kama wakishindwa hatua hizo mbili baasi angalau wanune na kukasirika kuonesha kwamba hawaungi mkono vitendo hivyo. Askofu Bagonza amesema katika maeno yote hayo viongozi wa dini hawajafanya vya kutosha.
Kwa mujibu wa Askofu Bagonza, sababu zinazowafanya viongozi wa dini washindwe kutekeleza wajibu wao huo, ni pamoja na viongozinwa dini kuwa sehemu ya uongozi wa kitaifa. “Sisi ni sehemu ya mfumo unaotawala kwa hiyo kusema sema na kupinga pinga na kukosoa kosoa wakati sisi ni sehemu ya ule mfumo unaotawala” amesema.
Sababu nyingine amesema ni malezi ya kidini yanayosisitiza katika utii usiohojiwa, kwa hiyo mtu baada ya kuambiwa kutii miaka yote, unalemaaa na kupoteza uwezo wa kuhoji.
Askofu Bagonza amesisitiza kwamba yeye hawezi kuacha kupigania masuala ya haki kwa sababu akiacha kufanya hivyo anaweza kuathirika. “Naathirika kwa sababu kuongoza watu wasiokuwa na furaha, kuongoza watu ambao hawatendewi haki, kuongoza watu ambao wanadhulimiwa, sioni kama ni sawa sawa” Amesema.
Pia alisema kwamba viongozi waliomlea kidini na kijamii walimuandaa vyema kisiasa. Alimtaja Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere kama mmoja wa ‘role models’ wake waliomuandaa vyema.
Aliongeza “Kanisa ninaloliongoza (KKKT) likiacha kutetea haki litakuwa sio kanisa like ka Yesu Kristo Mnazareth aliyezaliwa katika maisha dhuluma lakini akatoa sauti kukataa dhuluma”