Dar es Salaam.
Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Tadheus Ruwai’chi ameagiza mapadri wote wa jimbo hilo kupata chanjo dhidi ya Uviko 19 kwa kuwa ugonjwa huo unaumiza na kuondoa uhai.
Ametoa agizo hilo leo Jumanne Agosti 24, 2021 katika adhimisho la Misa Takatifu ya kumuombea Padri Paul Haule aliyekuwa Paroko Msaidizi katika Parokia ya Mtakatifu Petro na Mkurugenzi wa Tumaini Media.
Ruwai’chi amesema mwaka 2020 wakati wa awamu ya kwanza ya janga la Uviko-19 watu walimuomba Mungu ajaalie kupatikana kwa chanjo, ambayo sasa imepatikana.
“Tulimuomba Mungu ajaalie kupatikana kwa chanjo sasa imepatikana badala ya kutumika watu wameingia katika malumbano ya kusema haya na yale dhidi ya chanjo,” amesema.
“Tusingojee hadi mambo haya yatutinge, tutumie vizuri fursa alizotupa Mungu kujikinga na kujihami na kwa sababu hiyo, sijui ni mapdri wangapi ambao mmeshachanjwa, lakini leo naomba nitoe agizo, kila padre akachanjwe, kila padre akachanjwe, tusifanye utoto, tusifanye lelemama, hii uviko 19 haina mjomba na shemeji na inatuondolea uhai,” amesema Ruwai’chi.
COMMENTS