Wananchi wa Kijiji cha Nambogo Manispaa ya Sumbawanga, wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kusaidia kukamilisha ujenzi wa zahanati yao iliyoanza kujengwa mwaka 2000 na kukamilika mwaka huu.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa zahanati hiyo jana Novemba 5, 2022, kwa niaba ya wananchi Mzee Lemeli Mbalamwezi (86) ambaye ndiye alitoa eneo hilo alisema wanaishukuru serikali kwa kutoa fedha zilizosaidia mradi huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zahanati hiyo, Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Queen Sendiga, ameipongeza Manispaa ya Sumbawanga kwa kutekeleza maelekezo yake aliyoyatoa Oktoba 05 mwaka huu alipokagua zahanati hiyo kuwa watoe fedha za mapato ya ndani kukamilisha kazi iliyoanzishwa na wananchi miaka 22 iliyopita.
“Watumishi wenzangu wa serikali mkiniona kwenye maeneo yenu msinune kwani Rukwa bila miradi ya viporo inawezekana. Tusiishi kwa presha, tufanye kazi na kutimiza wajibu wetu wa kuhudumia wananchi,” amesisitiza RC Sendiga.