Baraza la amani na usalama limesaidia kukabiliana na ugaidi Afrika

HomeKitaifa

Baraza la amani na usalama limesaidia kukabiliana na ugaidi Afrika

Rais Samia Suluhu hassan amesema Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika(AU) limezisaidia nchi za Afrika kujilinda dhidi ya matishio ya kiusalama ikiwemo ugaidi.

Baraza la Amani na Usalama ni chombo cha juu cha maamuzi kuhusu masuala ya amani na usalama kwenye Umoja wa Afrika likiwa na jukumu la kuzuia kutokea kwa migogoro, kusuluhisha au kukabiliana nayo pale inapojitokeza.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya baraza hilo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam leo Mei 25, 2024 amesema mbali na kujlinda dhidi ya ugaidi baraza hilo lililooanzishwa mwaka 2004 limezisaidia nchi za Afrika hususani zilizokabiliwa na vita kujiimarisha.

“Tangu kuanzishwa kwake baraza limepata mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzishwa majadiliano ya upatanishi hadi kusaidia nchi kujengwa upya baada ya vita (Post war),” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia aliwaambia wahudhuriaji kuwa baraza hilo hilo limejidhatiti katika kusimamia misingi ya haki za binadamu, demokrasia na utawala bora, pamoja na kuangazia ushirikishwaji wa wanawake na vijana katika masuala ya amani na usalama.

Maadhimisho hayo yanafanyika nchini Tanzania ikiwa bado kuna nchi barani Afrika zinakabiliwa na na machafuko ya kisiasa yanayopelekea watu kupoteza maisha ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Somalia na nyinginezo ambapo Rais Samia ameitaja hali hiyo kama changamoto inayolikumba baraza hilo.

“Tumeshuhudia migogoro ya uhalifu wa kimataifa na ukosefu wa hatua madhubuti za kuizuia, kwa ujumla bado hatujanyamazisha kabisa bunduki barani Afrika, changamoto nyingine kubwa ni mabadiliko ya kikatiba ya Serikali na urejeshaji wa utaratibu wa kikatiba,” amebainisha Rais Samia.

Awali Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU ) Moussa Faki Mahamat alifafanua changamoto ya kikatiba kuwa miongoni mwa sababu zinazofanya baadhi ya chaguzi Afrika kukosa uangalizi kutoka baraza hilo kutokana na nchi wanachama kushindwa kutoa ratiba ya tarehe za uchaguzi kwa wakati.

Pia amesema changamoto nyingine ni nchi za Afrika kuingiliwa kimaamuzi na mataifa ya nje, hatua inayosababishwa na kukosekana kwa umoja na ushikamano baina ya nchi wanachama.

Pamoja na kuwepo kwa changamoto hizo Rais Samia amewataka wahudhuriaji wa maadhimisho hayo kujikita katika kutafuta suluhu ya changamoto hizo na kuzitatua.

error: Content is protected !!