Benki ya Dunia yaipongeza Tanzania kuwa kinara kwenye uchumi

HomeKimataifa

Benki ya Dunia yaipongeza Tanzania kuwa kinara kwenye uchumi

Huenda unafuu wa maisha pamoja na upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii ukaimarika nchini mara baada ya Benki ya Dunia kuripoti kuwa uchumi wa Tanzania unaimarika kwa kasi zaidi kuliko mataifa yote yaliyopo kusini mwa Jangwa la Sahara.

Benki hiyo katika ripoti yake ya hali ya uchumi wa Tanzania toleo la 18 ambayo imezinduliwa hii jana Februari 13, 2023 imeeleza kuwa baada ya kuathirika na janga la Uviko-19 kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni ya kuridhisha ingawa inakabiliwa na vita ya Urusi na Ukraine.

“Hatua za kiuchumi zilizochukuliwa zimeifanya kasi ya ukuaji kuwa katika hali nzuri ingawa bado inakabiliwa na athari za vita inayoendelea ya Urusi na Ukraine, “ inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, uchumi wa mataifa ya kusini mwa Jangwa la Sahara mwaka 2020  ulishuka kwa asilimia mbili huku waTanzania ukisalia palepale na kisha ukaongezeka kwa asilimia 4.3 mwaka 2021 na kuzidi wastani wa ukuaji kwa nchi hizo ambao ulikuwa kwa asilimia 4.2.

Ripoti hiyo imebainisha kwamba kasi ya ukuaji uchumi imekuwa kubwa zaidi katika miezi tisa ya mwanzo ya mwaka 2022 ambayo imechochewa na ukuaji wa sekta binafsi, kuimarika kwa sekta ya utalii, kukua kwa biashara pamoja na matumizi ya Serikali.

Kwa mujibu wa ofisi ya Taifa ya Takwimu NBS mwaka 2022 umerekodi kiwango kikibwa zaidi cha watalii tangu mlipuko wa janga la Uviko-19 utokee ambapo jumla ya watalii 1.45 milioni waliingia nchini ukilinganisha na watalii 922,692 walioingia nchini mwaka 2021.

error: Content is protected !!