Benki ya Dunia yatoa mkopo wa zaidi ya bilioni 700 kwa Tanzania

HomeKitaifa

Benki ya Dunia yatoa mkopo wa zaidi ya bilioni 700 kwa Tanzania

Huenda tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama vijijini  likapungua nchini Tanzania baada ya Benki ya Dunia kuidhinisha mkopo wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 300 sawa na Sh700.03 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya upatikanaji wa huduma hiyo.

Mkopo huo wa Mpango Endelevu wa Ugavi wa Maji Vijijini na Usafi wa Mazingira (SRWSSP) utasaidia upanuzi wa mpango huo kutoka halmashauri za wilaya 86 katika mikoa 17 hadi halmashauri za wilaya 137 katika mikoa 25 nchini.

Mpango huo utawezesha  shule za msingi za umma 1,850 na vituo 2,600 vya huduma za afya (HCFs)  kuboreshewa huduma za usafi wa mazingira. Ufadhili huo pia utasaidia majaribio ya skimu 206 za maji ambazo zitajengwa na Serikali na sekta binafsi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, Nathan Belete amesema benki hiyo imeridhishwa na matokeo ya ufadhili wa awali ambapo watu milioni 3.3 walifikiwa.

“Tunatiwa moyo sana na matokeo ya ufadhili wa awali wa programu ambayo zaidi ya watu milioni 3.3 walipatiwa huduma ya maji bora na maendeleo makubwa katika upatikanaji wa vyoo kwa kaya, shule na vituo vya afya,” amesema Belete katika taarifa ya benki hiyo iliyotolewa Disemba 14, 2022.

Mkopo wa awali wa dola milioni 350 kwa ajili ya SRWSSP uliidhinishwa Juni 2018, lengo likiwa ni kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji na usafi wa mazingira vijijini katika wilaya zinazoshiriki na kuimarisha uwezo wa taasisi za sekta teule ili kuendeleza utoaji wa huduma.

Utekelezaji wa mpango huo ulianza mwaka 2019 kwa kusaidia uanzishwaji wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), kama wakala maalumu wa utoaji huduma za maji vijijini.

Waziri wa Maji Juma Aweso alipokuwa akisoma hotuba nya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2022/23 aliwaambia wabunge kuwa upatikanaji wa huduma ya maji vijijini imefikia wastani wa asilimia 74.5 na lengo ni kufikia asilimia 85 mwaka 2025.

error: Content is protected !!