Bodi ya Mikopo kufungua dirisha la mikopo elimu ya juu Juni 15

HomeKitaifa

Bodi ya Mikopo kufungua dirisha la mikopo elimu ya juu Juni 15

SERIKALI imetangaza kuwa miongozo ya mikopo ya elimu kwa mwaka wa masomo 2025/2026 itapatikana katika lugha za Kiingereza na Kiswahili kwenye tovuti za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (www.moe.go.tz) na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (www.heslb.go.tz).

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo ametoa tangazo hilo leo Juni 6, 2025 jijini Dodoma.

Amesema dirisha la maombi kwa njia ya mtandao litafunguliwa kuanzia Juni 15 hadi Agosti 31, 2025, na kuwahimiza wanafunzi, wazazi na walezi kuisoma miongozo hiyo kwa siku 10 kabla ya kuanza mchakato wa kuomba.

Prof amesema mwaka huu, kama ilivyokuwa mwaka wa 2024/2025, waombaji hawatalazimika kutuma nakala ngumu za maombi kutokana na maboresho ya mfumo kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

Aidha, miongozo inasisitiza kuwa kila mwombaji awe na akaunti ya benki kwa ajili ya malipo chuoni na namba ya simu iliyosajiliwa ili kupokea ujumbe muhimu kutoka Bodi ya Mikopo.

Katibu Mkuu huyo amesema tarehe ya kufungua dirisha la maombi ya ruzuku ya Samia Scholarship itatangazwa baada ya NECTA kutangaza matokeo ya kidato cha sita mwaka 2025.

Serikali inaendelea kurahisisha taratibu za utoaji wa mikopo ili kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma kwa haraka na kwa ufanisi.

error: Content is protected !!