Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) umesema mwaka huu utaongeza mabasi mengine mapya 95 ikiwa ni sehemu ya hatua za kupunguza msongamano wa abiria kwenye vituo vya mabasi hayo.
Dk. Edwin Mhede ambaye ni Mtendaji wa Wakala huo alibainisha hayo jana wakati akifungua mafunzo kuhusu mipango ya mitaa kwa jiji la Dar es Salaam.
“Kabla ya mwisho wa mwaka huu tunakusudia kuongeza mabasi mengine mapya 95 na tunaamini kwa kufanya hivi tutaondoa kabisa muda wa kusubiri kwa sababu maana ya kuwapo kwa mabasi haya ni watu kuwahi makazini,” alisema Dk. Mhede.
Aidha, Dk. Mhede aliwaomba wananchi kuacha tabia ya kukatisha kwenye njia za DART kwa kuwa si salama kwao na kwa mabasi, akionya kuwa wananchi wengi wamekuwa wakipata majeraha wanapokatisha kwenye njia hizo.
“Hakuna haja yakukimbilia basi, ukakatisha njia ya UDART uwezekano wa kugongwa ni mkubwa. Sasa ni muhimu ukazingatia usalama wako kwanza kabla ya kuchukua uamuzi wa kukatisha kwenye njia hizo,” alionya Dk. Mhede.