Dkt. Mpango asisitiza wananchi kuliombea taifa

HomeKitaifa

Dkt. Mpango asisitiza wananchi kuliombea taifa

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 22 Julai 2022 ameshiriki ibada ya kawaida ya asubuhi katika Kanisa kuu katoliki la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili Jimbo la Mpanda mkoani Katavi. Ibada hiyo imeongozwa na Paroko Msaidizi Padri Leonard Kasimila.

Akizungumza na waumini mara baada ya kumalizika kwa ibada hiyo, Makamu wa Rais amewaomba waumini na viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa na viongozi wake ili waweze kuwatumikia wananchi jinsi inavyompendeza Mungu na kufikia hatua ya juu zaidi ya maendeleo. Aidha amewasihi kuendelea kuliombea taifa amani kwa kuwa bila uwepo wa amani hakutakuwa na maendeleo yeyote.

Pia Makamu wa Rais amewaasa waumini wa kanisa hilo kujitolea kikamilifu katika kutunza mazingira ilikuepukana na athari mbaya zinazoweza kujitokeza kutokana na uharibifu wa mazingira. Amewaagiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ili kuwa na jamii bora itakayoweza kuliendeleza vema taifa.

Makamu wa Rais yupo mkoani Katavi kwa ziara ya kikazi ambapo anakagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero na changamoto za wananchi katika mkoa huo.

 

error: Content is protected !!