Isaac Abraham Sepetu alizaliwa Oktoba, 15 1943 nchini Tanzania (Tanganyika) mkoani Tabora. Balozi Isaac Abraham Sepetu ni moja kati ya wasomi mahiri na bingwa wa kuzungumza kwa ufasaha lugha kubwa tatu adhimu za kimataifa, kikiwemo Kiswahili, Kiingereza na Kijerumani.
Balozi Sepetu ana sifa lukuki, lakini kwa uchache tu, mwaka 1972, Rais Julius Nyerere alimteua kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wadhifa aliodumu nao kwa miaka mitano (1972 -1977). Alikuwa Waziri wa Habari na Utangazaji kwa miaka miwili (1977 -1979), Waziri wa Utalii na Maliasili kwa miaka mitatu (1979 -1982).
Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Moscow kwa miaka saba (1982 – 1989) na Balozi wa Tanzania nchini Zaire sasa ikiitwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kwa mwaka mmoja (1989 -1990).
Balozi Isaac Abraham Sepetu aliwahi kuiwakilisha Tanzania katika Baraza la Umoja wa Mataifa Septemba 26, 1975. Aliutoa hotuba majira ya 9:15 Alasiri katika kikao cha 2364 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Kati wa wahutubi watatu wa siku hiyo, Balozi Sepetu alikuwa ni mzungumzaji wa tatu baada ya wazungumzaji wawili, kutoka Ufaransa na Norway.
Hotuba ya Balozi Sepetu ilikijita sana katika mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika dhidi ya ukoloni Kusini mwa Jangwa la Sahara, kupinga sera za ubaguzi wa rangi Afrika Kusini na kuhamasisha mataifa yaliyokuwa na ambayo yametoka kupata uhuru wakati huo, kuungana kupinga ukoloni na kujitegemea.