Anguko kwenye mtihani wa uwakili katika Shule Kuu ya Sheria Tanzania (LST) limefikia hatua mbaya na kuwaibua wanasheria na wadau wakitaka utafiti ufanyike kubaini chanzo cha tatizo hilo.
Katika idadi ya wanafunzi 633 waliotarajiwa kuhitimu Law School mwaka huu ni wanafunzi 26 pekee ndio wamefanikiwa kufaulu na 342 watatakiwa kurudia masomo (supplementary) na wanafunzi 265 wameondolewa (discontinued ).
Akijibu hoja hizo, Makamu Mkuu wa Chuo (Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo na Utafiti) , Profesa Zakayo Lukumay alisema tatizo kubwa linatokana na namna wanafunzi walivyoandaliwa katika vyuo walivyotoka.
“Waliofundishwa na walimu wazuri wanafaulu, lakini waliofundishwa vibaya ndiyo hao wanaofeli kwa kuwa wanakuja na uelewa mdogo ilhali asili ya mafunzo yetu ni kufanya kwa vitendo,” alisema.
Alisema kwenye shule hiyo kinachofundishwa ni jinsi ya kuifanya kazi ya taaluma husika, mathalan namna ya kumuhoji shahidi na kuandaa nyaraka za kisheria, wakiamini kuwa tayari mwanafunzi huyo alishafundishwa maana ya shahidi.
“Kule chuoni alijifunza kitu kinachoitwa hukumu, kinatakiwa kuwaje, lakini huku shule ya sheria tunamtaka aandike huku,” alisema Profesa Lukumay.
Alisema wanaofeli wengi wao, hawajui kufanya vile walivyoelekezwa kwa nadharia.