Hatimaye Serikali imefanikiwa kuishusha majini meli mpya itakayokuwa ni kubwa kuliko zote ndani ya Victoria ya Mv.Mwanza “Hapa kazi tu” baada ya ujenzi wake kukamilika kwa hatua ya pili ya asilimia 82.
Meli hiyo yenye urefu wa mita 92.6, kimo cha mita 20 na upana wa mita 17 imeshushwa leo February 12, 2023 ikiwa ni miaka minne tangu ilivyoanza kujengwa Januari 2019 jijini Mwanza.
Hadi kukamilika kwake, meli hiyo itakuwa na uzito wa tani 3,500 ikiwa ni ongezeko la tani 500 zaidi kutoka tani 3,000 zilizorekodiwa leo wakati ikishushwa majini ndani ya Ziwa Victoria.
Baada ya kukamilika na kuanza safari, meli hiyo itakuwa kubwa kuliko zote katika Ziwa Victoria.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya huduma za meli nchini (MSCL) Erick Hamis ameeleza jana baada ya zoezi la ushushaji wa meli hiyo kukamilika kuwa kilichofanyika ni hatua muhimu ya pili katika ujenzi wa meli hiyo.
Amesema sehemu kubwa ya ujenzi wa meli hiyo imefanywa na Watanzania kwa asilimia 100 wenye umri wa kati ya miaka 21 hadi 35 ambao walishirikiana na wakandarasi sita (6) kutoka nje ya nchi.
Kuhusu Meli ya Mv. Mwanza
Meli hiyo ya Mv. Mwanza ina uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo na magari madogo 20.
Ndani kutakuwa na madaraja sita yatakayoanza na daraja la VVIP litakalokuwa maalum kwa viongozi wa kitaifa ambao watakuwa wanakaa watu wawili tu wakati daraja linalofuata la VIP litabeba watu mashuhuri likihusisha watu wanne tu yaani vyumba vine.
Daraja la kwanza litahudumia watu 60, daraja la biashara litakuwa na uwezo wa kuhudumia watu 100 na daraja la pili litakalokuwa na watu 200.
“Daraja la mwisho kwenye meli hii litakuwa ni la uchumi ambalo litakuwa minabeba abiria 834 na katika daraja hili kutakuwa na hadhi ya kisasa na wananchi watakaa kwa starehe na wataweza kufanya utalii,” amesema Hamis.
Ndani ya meli hii pia kutakuwa na buradani mbalimbali na kutakuwa na sehemu ya lift hasa kwa watu wenye changamoto ya kupanda ngazi na wagonjwa, na sehemu ya hospotali (dispensary) na sehemu ya kina mama wajawazito.
“Tunatarajia meli hii itakuwa inatumia saa 10 pekee kwenda bandari ya Portbell nchini Uganda lakini pia itaenda Musoma mkoani Mara,” amesema Hamis.
Hata hivyo, nauli ya meli hii zitafahamika baada ya kukamilika na kupewa cheti cha ubora na Tasac.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema Serikali iliamua kujenga meli kubwa ili kukidhi mahitaji ya soko ambayo yanatarajiwa kuongezeka hasa baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Kujengwa kwa meli hiyo, amesema kutasaidia kufungua masoko mapya ndani na nje ya nchi kwa kuanzisha safari mpya zitakazosaidia kurahisisha shughuli za kibiashara, kikazi, utalii na safari binafsi kwenye maeneo mengi zaidi ilivyo sasa.
Waziri huyo pia amepongeza kitendo cha kampuni hiyo kwa kutoa fursa za ajira kwa vijana wengi wakitanzania ambapo takribani watanzania 3,000 waliajiriwa katika mradi huu pamoja na chelezo lililotumika kujenga meli hiyo.
Mbali na hao, Watanzania wengine 2,000 wameajiriwa kwenye miradi mingine ya ukarabati wa meli.