Fahamu kwa nini leo ni ‘Ijumaa Nyeusi’

HomeMakala

Fahamu kwa nini leo ni ‘Ijumaa Nyeusi’

Leo ni ‘Black Friday’ (Ijumaa Nyeusi), siku ambayo bidhaa katika maduka na mitandao mbalimbali hususan nchini Marekani, zinapatikana kwa bei chee.

Kwa nini Ijumaa ya leo iwe Nyeusi (Black Friday)?

Sababu kubwa ya kufanya Ijumaa ya leo iwe ‘Black Friday’ ni utamaduni wa Wamarekani, ambao ulipewa baraka na Serikali yao ambapo waliamua kwamba Ijumaa baada ya Alhamisi inayotumika kwa ajili ya kutoa shukrani (Thanksgiving) iwe siku ambayo bei ya bidhaa zinashushwa.

Zipo nadharia nyingi kuhusu historia halisi ya ‘Black Friday’, lakini wengi wanakubaliana kwamba jambo hilo lina uhusiano na kuanguka kwa bei ya dhahabu nchini Marekani kulikotokea Septemba 24 mwaka 1869.

Mwaka 1869, wafanyabiashara wawili, Jay Gould na Jim Fisk walificha dhahabu nyingi, na kuweza kusababisha bei ya dhahabu nchi Marekani kupanda. Tovuti ya History.Com inaeleza kwamba baadae Rais Ulysses Grant aliharibu mipango ya wafanyabiashara hao kwa kuacha kiasi kikubwa cha dhahabu kiingie kwenye mzunguko.

Uwepo wa dhahabu nyingi sokoni ulifanya bei ya madini hayo iwe chini sana, na huo ndio ulikuwa mwanzo wa ‘Black Friday’ ambayo baadae ilihusisha kushuka kwa bei za bidhaa nyingine badala ya dhahabu pekee.

Wakati mwingine ambapo jina ‘Black Friday’ lilitumika zaidi ni miaka ya 1950 katika mji la Philadelphia. Watu katika mji huo walikuwa wanapenda sana mchezo mpira wa Kimarekani (Army-Navy Football Game) ambao ulikuwa ukifanyika siku ya Jumamosi.

Siku moja kabla ya Jumamosi ya mchezo huo, yaani Ijumaa, ilikuwa na matukio ya watu kujaa kwenye maduka kutafuta bidhaa mbalimbali, wengine wakiib na kuvunja maduka. Jambo hilo liliwafanya Polisi wa mji huo waichukie siku hiyo na kuipa jina la ‘Black Friday’ (Ijumaa Nyeusi) kwani walikuwa wanapata kazi ya ziada kupambana na uhalifu.

Pamoja na nadharia nyingi ambazo zinaweza kukinzana kuhusu asili ya ‘Black Friday’, jambo la hakika ni kwamba Alhamisi ya mwisho ya mwezi Novemba, ilitangazwa rasmi kuwa siku ya kutoa shukrani (Thanksgiving) mwaka 1942 nchini Marekani chini ya Rais Franklin Delano Roosevelt. Katika karne ya 20, ulizuka utaratibu wa kufanya Ijumaa baada ya Alhamisi ya ‘Thanksgiving’ iwe siku ya kufanya manunuzi kwa bei chee.

Utamaduni huo ulioanzia nchini Marekani umesambaa katika mataifa mbalimbali duniani, ambapo ‘Black Friday’ inatumika kama mwanzo wa kufanya manunuzi kwa ajili ya msimu wa sikukuu za mwezi Desemba.

error: Content is protected !!