Fedha za Uviko kuzalisha shule maalum Tanga

HomeKitaifa

Fedha za Uviko kuzalisha shule maalum Tanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amesema utekelezaji wa miradi mbalimbali kupitia fedha za mpango wa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19 umewapa wazo la kuanzisha shule za sekondari maalum tatu.

Miradi hiyo imetekelezwa kwa sehemu ya fedha za mkopo wa masharti nafuu wa Shilingi trilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa ajili ya utekelezaji wa mapambano ya Uviko-19, ambapo Serikali ya Tanzania iliamua kuzielekeza katika utatuzi wa changamoto katika sekta za elimu, afya na maji.

Malima aliyasema hayo hivi karibuni wakati akielezea mafanikio ya fedha hizo zilizokwenda kutatua changamoto mbalimbali katika mkoa wake hasa katika sekta ya elimu iliyojenga na kuboresha vyumba vya madarasa katika shule za sekondari na msingi.

Akiwa katika ukaguzi wa shule mpya ya sekondari ya Saruji iliyopo wilayani Tanga Mjini, Malima alisema fedha za Uviko-19 zimechangia kwa kiasi kikubwa kujengwa kwa shule hiyo yenye vyumba vya madarasa 14.

“Kutokana na fedha hizi za Uviko-19, tumekuja na wazo jingine la shule hii iwe shule maalum. Sasa itakuwa na mabweni, viwanja vya michezo mbalimbali ili wale wanafunzi wenye vipaji na mahitaji maalum waje kusoma hapa na kuendeleza vipaji vyao.

“Kwa mkoa wa Tanga, tunataka kuwa na shule tatu katika wilaya ya Tanga Mjini itakayochukua wanafunzi kutoka Pangani, Mkinga na Muheza. Pia, tutajenga Handeni ambayo itachukua wanafunzi wa kutoka Kilindi na tunafikiria kujenga pia katika wilaya ya Lushoto au Korogwe,” alisema Malima.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kazi kubwa iliyofanyika kwenye shule ya Saruji imewapa msingi viongozi wa mkoa huo kuja na wazo la kuwa na shule maalumu tatu huku akisema ujenzi wa vyumba vya madarasa uliofanyika ndani ya muda mfupi umetatua kero mbalimbali za watoto ikiwemo umbali.

Alifafanua kuwa vituo vya afya vilivyojengwa kutokana na fedha za miamala ya tozo pamoja na ujenzi wa madarasa umezingatia mahitaji mahsusi ya wananchi kwa maeneo husika ili kuwapungumzia mzigo wa gharama na changamoto mbalimbali walizokuwa wakikabiliana nazo.

“Fedha za tozo na Uviko-19 zimekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha miundombinu na kurahisisha huduma kwa wananchi. Tunaishukuru Serikali kwa kuipa Tanga zaidi ya Shilingi bilioni 20 zilizotokana na tozo, Uviko-19 pamoja na fedha za miradi ya maji,” alisema.

“Uwekezaji katika sekta ya elimu, afya na maji umeleta ahueni kubwa wananchi wa Tanga. Fedha za tozo zimesaidia kujenga vituo vya afya zaidi ya 12 pamoja na kukamilisha maboma ya shule 50 kwa gharama ya milioni 12 kwa kila moja,” alisema.

Awali, mkuu wa wilaya ya Muheza, Halima Bulembo aliishukuru Serikali kwa kuwapatia sehemu ya fedha za IMF na tozo zilizoelekezwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo, ujenzi wa vyumba vya madarasa na vituo vya afya.

Alisema katika wilaya ya Muheza walijenga madarasa 10 ya vituo vitatu shikizi ambayo hayakuwepo huku akisema ndani ya miezi mitatu mchakato huo umekamilika. Alisema uandikishaji kwa mwaka huu umekuwa mkubwa, kila mtoto amepata fursa ya kuanza darasa la kwanza au kidato cha kwanza.

error: Content is protected !!