Fidia kulipwa kwa wakazi wa Bonde la Msimbazi

HomeKitaifa

Fidia kulipwa kwa wakazi wa Bonde la Msimbazi

Zaidi ya wananchi 11,000 wanatarajiwa kulipwa fidia Januari mwakani kupisha ujenzi wa daraja la juu la kisasa la Jangwani na uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi mkoani Dar es Salaam.

Wananchi hao watakaonufaika ambao bajeti yake ya fidia imeshatengwa ni wenye nyumba, wamiliki wa ardhi na wapangaji ambapo katika eneo hilo la Bonde la Mto Msimbazi kutajengwa ‘City Park’ na daraja la juu la kisasa.

Akizungumza Dar es Salaam, Mratibu wa miradi ya Benki ya Dunia, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Humphrey Kanyenye alisema nyumba zitakazolipwa fidia ni 3,291 na wapangaji wenye mikataba.

“Taratibu za kulipa fidia kwa watu zaidi ya 11,000 na nyumba 3,291, wamiliki wa ardhi na wapangaji wenye mikataba zimekamilika na matarajio Januari, mwakani hatua hiyo itaanzwa kwa kuzingatia sheria,” alisema.

Kanyenye alisema kwa kuwa tathmini inaendelea, gharama za malipo ya fidia bado hadi hatua hizo zitakapokamilika. “Wote watalipwa kupisha huu mradi, serikali imejipanga, fedha zipo, mchakato umeanza kwa kushirikisha kamati za mitaa, kata na kijiji…nyumba zitalipwa kutokana na thamani, ardhi hata wapangaji wenye mikataba wamefanyiwa tathmini watalipwa, lengo ni kuwawezesha kumiliki ardhi sehemu nyingine.

Tathmini inaendelea na huenda ikafika hadi eneo la Kigogo,” alisema na kuongeza: “Serikali imepanga kurudisha uoto wa asili katika eneo hilo, kwa kujenga ‘City park’ kubwa ya kisasa kama Ulaya ambapo hekta zilizopo 420 kwa eneo lote, zinatosha kufanya kuwa sehemu ya tofauti yenye vivutio vingi.”

Alisema tayari kampuni kubwa zimeanza kujitokeza na mazungumzo yanaendelea wakitaka kuwekeza pembezoni mwa mto, hali itakayofanya kuwa na vivutio vya aina yake na uwekezaji utakaofanyika unatosha kulipa fedha za mkopo zilizotolewa na Benki ya Dunia kukamilisha mradi.

error: Content is protected !!