Siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kurekodi kipindi cha kuhamasisha utalii wa Tanzania maarufu kama ‘Royal Tour,’ mawakala wa utalii zaidi ya 30 kutoka nchini Marekani, Ufaransa na Lithuania wamehamasika kutembelea nchini ili kujifunza na kujionea vivutio vya utalii vilivyopo.
Mawakala hao wanatarajia kuingia nchini Novemba 23 mwaka huu na kukaa kwa muda wa siku saba, kwa lengo la kutembelea vivutio hivyo na maeneo mbalimbali ya uwekezaji.
Hayo yote yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Francis Malugu kutoka kampuni ya kimataifa inayojihusisha na masuala ya utalii ya Kilimanjaro International Tourism & Safaris (KITS).
Malugu amesema mafanikio ya ujio wa mawakala hao yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na hatua ilizochukua kampuni hiyo, baada ya kuona taarifa za Rais Samia akishiriki kutengeneza kipindi hicho cha kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania.
“Mara baada ya kupata taarifa mapema za utengenezaji wa makala hiyo ya filamu na kwamba Rais Samia ndiye atakayekuwa mwongozaji mkuu, tuliwataarifu mawakala wa utalii katika vyama vya utalii duniani ambavyo KITS ni mwanachama wake na zaidi ya mawakala 30 waliomba na kuthibitisha kuja kuitembelea Tanzania, Novemba mwaka huu.”
Ameongeza kuwa wakifika wanatarajia kutembelea vijiji vya Masai mkoani Arusha, Hifadhi ya Serengeti, Tarangire na Hifadhi ya Arusha.