Hoteli ya nyota 5 itakayojengwa Dodoma

HomeBiashara

Hoteli ya nyota 5 itakayojengwa Dodoma

Jiji la Dodoma linatarajia kuwa na hoteli yenye hadhi ya nyota tano ifikapo mwaka 2024 baada ya kampuni ya ‘Louvre Hotels Group’ (Golden Tulip) kuweka wazi mpango wake wa kujenga hoteli hiyo.

Rais wa Golden Tulip Africa amesema wanatarajia kujenga hoteli hiyo kwa ushirikiano na kampuni za Kifaru Group na Indian Ocean Hotels Limited ambapo ujenzi huo utagharimu takribani shilingi za Kitanzania bilioni 46.

Hoteli hiyo itakayojengwa katika eneo la Ndejengwa itakuwa  na vyumba 100, ukumbi mkubwa wa mikutano na maeneo mengine ya kuvutia.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ‘Indian Ocean Hotels’, Jitesh Ladwa amesema wameamua kufanya uwekezaji huo mkubwa kutokana na ukuaji mzuri wa uchumi wa Tanzania na sera nzuri zinazowekwa chini ya Rais Samia Suluhu.

“Rais Samia anaweka sera nzuri zinazovutia wawekezaji na ndio maana tumeshawishika kuongeza uwekezaji wetu hapa Tanzania” amesema Jitesh Ladwa.

Aidha hoteli hiyo inatarajiwa kutengeneza ajira za 200 za moja kwa moja na ajira 2,000 zisizo za moja kwa moja.

Kampuni inayojenga hotel hiyo inamiliki pia hotel ya Golden Tulip iliyopo jijini Dar es Salaam pamoja na hoteli nyingine zaidi ya 1,500 katika nchi 54 ulimwenguni.

 

error: Content is protected !!