Huduma kwa wateja TANESCO kutolewa kidigitali

HomeKitaifa

Huduma kwa wateja TANESCO kutolewa kidigitali

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limegeukia fursa kuboresha ufanisi kwa kutumia digitali, baada ya kusaini mkataba na Kampuni ya Tech Mahindra kwa ajili ya ujenzi wa Mfumo wa Usimamizi Rasilimali na Mipango ya Shirika (CMS).

Mkataba huo umesainiwa leo, Novemba 9, 2021, Makao Makuu ya Tanesco, Dodoma.

Tarifa kutoka inaeleza kwamba, Shirika hilo katika majukumu yake ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme kwa sasa inageukia fursa za kidijitali kwa kutumia wigo wa teknolojia kuboresha huduma kwa Wateja.

Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Maharage Chande alisema kusainiwa kwa mkataba huo ni muhimu ili Tanesco ifanikishe ufanisi ambao ni miongoni mwa vipaumbele 7 vya Tanesco, vipaumbele vingine ni rasilimali watu, wateja, miradi ya kimkakati, kutafuta rasilimali, mawasiliano na ushirikishaji wadau pamoja na viashiria vya hatari na utawala bora.

“Utekelezaji wa mfumo huu ni muhimu ili tufanye kazi yetu kwa ufanisi, sio tu kwa wateja wetu lakini pia kwa wafanyikazi wetu. Hii ni pamoja na kufanya shughuli zetu za msingi kuwa za kisasa na michakato yetu ya ndani kuwa rahisi, ili kuharakisha ubunifu tunaposonga mbele katika kuboresha huduma kwa wateja wetu” alisema Maharage.

“Katika kipindi cha miezi 30 ijayo, tutakuwa tukiendesha huduma zetu kidigitali, hii itatusaidia kuziona vyema rasilimali zetu na kupangilia kutokana na mahitaji. Aidha kutoa huduma yenye thamani na ubora kwa wateja wetu,” aliongeza Maharage.

Mkuu wa Afrika, Tech Mahindra, Prasad Kotikela alisema, “Lengo letu ni kuongeza kwa kiasi kubwa utayari wa TANESCO kutumia dijitali katika kuhudumia vyema wateja wake na wananchi wa Tanzania”
Kwa pamoja, TANESCO na Tech Mahindra zinalenga kuboresha wepesi katika utendaji kazi wa Tanesco huku wakiboresha mapato yatokanayo na uwekezaji kupitia mageuzi yanayoongozwa na teknolojia. Mkataba huo una thamani ya Dola Milioni 30.

error: Content is protected !!