Tanzania itakavyonufaika na ziara ya Rais Samia nchini Ufaransa

HomeKitaifa

Tanzania itakavyonufaika na ziara ya Rais Samia nchini Ufaransa

Mkurugenzi wa Mawasiliano-Ikulu, Bi. Zuhura Yunus alitoa taarifa siku ya jana Februari 9,2022 ikisema Rais Samia akiwa nchini Ufaransa atashuhudia utiaji saini mikataba baina ya serikali ya Tanzania na Ufaransa katika sekta za miradi ya maendeleo, ushirikiano katika masuala ya uchumi wa bluu, usalama wa bahari, sekta ya usafiri na maendeleo endelevu.

Rais Samia anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali utakaojadili kuhusu rasilimali bahari duniani( One Ocean Summit) ambao umeitishwa na rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, unaotarajia kufanyika kwa siku tatu pia utazingatia juhudi za kuboresha utawala wa bahari kuu na kuratibu utafiti wa kiyasansi wa kimataifa.

Mkutano huo  utayaleta pamoja makampuni makubwa ya meli kama Maersk, CMA CGM na Hapag-Lloyd, ambayo yanachukua karibu asilimia 55 ya mizigo ya baharini duniani, pamoja na wanasayansi wakuu, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO), watunga sera na mashirika ya kimataifa.

Siku mbili za kwanza za mkutano huo zitakuwa za warsha na vikao 30 vya umma juu ya mada mbalimbali ikiwemo sayansi ya baharini, Mediterania, meli endelevu, bandari za kijani, na miji iliyo katika hatari ya kuongezeka kwa viwango vya bahari, zitakazowaleta pamoja watafiti 300, wajasiriamali na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yakiwemo ya Umoja wa Mataifa (UN).

Mkutano huo wa ngazi ya juu utakaofanyika Ijumaa asubuhi utahusisha wakuu wa nchi na serikali kutoka mabara yote matano akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan.

Baada ya kukamilisha ziara nchini Ufaransa, Rais ataelekea Ubelgiji kwa ziara ya kiserikali.

Nchi hizo mbili zimekuwa na uhusiano wa karibu na Tanzania kwa muda mrefu katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na maji ambapo Tanzania imekuwa ikipata mikopo na misaada kuimarisha huduma za kijamii kwa ajili ya maendeleo ya raia wake

error: Content is protected !!