INEC Yaunda Majimbo Mapya 8 kwa Uchaguzi wa 2025

HomeSiasa

INEC Yaunda Majimbo Mapya 8 kwa Uchaguzi wa 2025

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeongeza majimbo mapya manane ya uchaguzi nchini, uamuzi utakaongeza ukubwa wa Bunge na kulifanya liwe na wabunge zaidi ya 400 baada ya Uchaguzi Mkuu hapo Oktoba mwaka huu.

Katika mkutano wake na wanahabari jijini Dodoma, jana Mei 12, 2025, Mwenyekiti wa INEC Jaji Jacobs Mwambegele amesema hatua hiyo imefikiwa kwa mujibu wa sheria baada ya kukaa na wadau wa baadhi ya majimbo yaliyoomba kugawanywa na kujiridhisha na taarifa za maombi zilizowasilishwa tume.

Majimbo nane yaliyoongezwa yanajumuisha mawili yaliyopo Mkoa wa Dar es Salaam ambayo ni Jimbo la Kivule lililogawanywa kutoka Jimbo la Ukonga, na jimbo la Chamazi lililogawanywa kutoka Jimbo la Mbagala.

Kwa mkoa wa Dodoma limeanzishwa Jimbo jipya la Mtumba lililogawanywa kutoka jimbo la Dodoma Mjini na Jimbo jipya la Uyole lililogawanywa kutoka Jimbo la Mbeya Mjini kwa mkoa wa Mbeya.

Majimbo mengine ni Jimbo la Bariadi Mjini kwa mkoa wa Simiyu, Jimbo la Katoro na Chato Kusini mkoani Geita, pamoja na Jimbo la Itwangi mkoani Shinyanga.

Pamoja na ongezeko la Majimbo ya Uchaguzi, tume hiyo pia imeongeza kata tano kwa upande wa chaguzi za madiwani na kufanya kufikia jumla ya kata 3,960 kutoka kata 3,955 zilizoshiriki uchaguzi mwaka 2020.

error: Content is protected !!