Kauli ya Serikali kuhusu ongezeka bei za vyakula

HomeKitaifa

Kauli ya Serikali kuhusu ongezeka bei za vyakula

Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa hakuna maeneo yatakayokosa chakula kwa kuwa inayo hifadhi ya kutosha huku ikisisitiza kuwa, bei ya bidhaa nyingi ikiwamo ya chakula ni nafuu Tanzania ukilinganisha na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Aidha, imesema ni kosa la kisheria kwa wafanyabiashara kupandisha kiholela bei ya bidhaa hasa vyakula hususani wakati wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya na kwamba mfanyabiashara anayefanya hivyo anaweza kushitakiwa kosa la uhujumu uchumi.

Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alisema hayo wakati akizungumzia mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini kwa mwezi Desemba 2022.

“Kupitia ushindani wa haki, kuna hatua mbalimbali dhidi ya anayekiuka na kupandisha bei kiholela ikiwamo kufutiwa leseni au kufikishwa mahakamani kwa kuwa huo ni uhujumu uchumi,” alisema Kigahe.

Kigahe alibainisha kuwa serikali inafanya juhudi mbalimbali kudhibiti mfumuko wa bei nchini ikiwamo kuweka ruzuku kwenye mafuta hali iliyopunguza gharama za usafirishaji na kupunguza baadhi ya kodi katika malighafi za uzalishaji bidhaa.

Alisema kutokana na juhudi hizo za serikali, bidhaa nyingi zikiwamo za chakula na vifaa vya ujenzi, ni nafuu ukilinganisha na baadhi ya nchi wanachama wa EAC.

“Mwenendo wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli duniani zinazochangia mfumuko wa bei umeendelea kuimarika na bei za bidhaa hizo zimeendelea kushuka na hivyo kupunguza gharama za uagizaji, usafirishaji na uagizaji wa bidhaa na malighafi zinazotumika katika uzalishaji kutoka nje ya nchi,” alisema.

error: Content is protected !!