Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo ya kuundwa kwa kikosi kazi cha taifa, ambacho kitaongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kitakuwa na kazi ya kuchakata na kutoa suluhu ya afua ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza leo Novemba Mosi, 2022 katika uzinduzi wa Kongamano la Kitaifa la kuhusu nishati safi ya kupikia, ameagiza kikosi kazi hicho kije na afua ambazo zitaweza kutekelezeka.
“Mpango huu nataka uratibiwe kitaifa, kuliko kila mmoja anafanya lake hatujui nani anafanya nini,” amesema Rais Samia na kuongeza:
“Suala hili ni mtambuka, linakata sekta zote, kuanzishwa kikosi kazi ambacho ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Madini kupitia Stamico, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Tamisemi zote ziungane na sekta binafsi tuone sekta binafsi wanaingiaje, watoe maoni yao.
“Msiwasahau pia wadau wa maendeleo, wadau wa maendeleo waje na ‘road map’, ambayo itatoa suluhu ya nishati safi na endelevu ya kupikia,”amesisitiza.
Rais Samia amesema kikosi kazi hicho kiongozwe na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kiratibiwe na Wizara ya Nishati wenyewe.
“Ni lazima twende na nishati safi ya kupikia kwa maendeleo ya nchi, kukinga na kulinda haki za wanawake, wanawake wana mambo mengi ya kujitolea ya kuumiza afya zao bila malipo.
“Tumeona filamu fupi wakina mama wanasonga ugali, macho yamejaa machozi kwa ajili ya moshi wa kuni, ukute watoto anaowatumikia wala hawamsaidii, nani anamlipa huyo mama? Amehoji Rais Samia na kuongeza …; “Nishati imsaidie mama.