Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linachunguza madai ya wananchi wa Kijiji cha Uchau, wilayani Moshi kuwa kumekuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwemo kupigwa na mauaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema wananchi wa eneo hilo wamelalamika kikundi kilichoanzishwa na diwani wa kata hiyo, Bahati Mambomba kinawapiga watu wanapokunywa pombe.
Wananchi wameeleza kuwa kikundi hicho kimesababisha kifo cha Patrick Kulaya (45) kwa kumpiga, na hivyo wakataka jeshi la polisi kuingilia kati.Maigwa amesema baada ya uchunguzi wakibaini madai hayo ni ya kweli, wahusika wote watachukuliwa hatua za kisheria.
Hata hivyo, diwani huyo amesema kuwa kikundi hicho kiliundwa kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya kudhibiti uhalifu na wazururaji na kwamba wanaolalamika ni wale wasiopenda maendeleo ya kijiji hicho.