Kila la heri darasa la saba

HomeKitaifa

Kila la heri darasa la saba

Watahiniwa milioni 1.4 wa darasa la saba wanatarajia kuanza mitihani ya kumaliza elimu ya msingi leo, ikiwa ni daraja muhimu kujiunga na sekondari.

Kwa mujibu wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) mitihani hiyo itafanyika kwa siku mbili Oktoba 5 hadi 6, 2022 nchi nzima.

Necta imesema kati ya watahiniwa hao, 723,064 ni wasichana sawa na asilimia 52 ya watahiniwa wote.

Idadi ya watahiniwa hao imeongezeka kwa asilimia 22 kutoka milioni 1.1 wa mwaka 2021.

“Aidha, jumla watahiniwa wenye mahitaji maalum ni 4,221, miongoni mwao 101 ni vipofu,  1,198 wasioona vizuri, viziwi 962, walemavu wa akili 487 na walemavu wa viungo 1,473,” amesema Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Athumani Amasi.

Mtihani huo utahusisha jumla ya masomo matano ambayo ni Hisabati, Sayansi na Teknolojia, Kiswahili, Lugha ya Kiingereza, na Maarifa ya Jamii.

Kwa mujibu wa Necta, ufaulu wa jumla wa wanafunzi katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana ulikuwa 81.97 huku wanafunzi 393 walifutiwa matokeo.

error: Content is protected !!