Serikali ya Jamhuri ya Korea imetoa mkopo wa gharama nafuu wa sh bilioni 310 kwa Tanzania kwa ajili ya upanuzi wa mfumo wa utambuzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na uendelezaji na utunzaji wa mfumo wa taarifa za ardhi.
Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo baina ya Serikali ya Tanzania na Korea Kusini itakayotolewa kupitia benki ya Exim ya Korea, imefanyika jana (Alhamisi, Oktoba 27, 2022) katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Korea Kusini iliyopo Seoul.
Mkataba wa awamu ya pili ya mradi wa upanuzi wa mfumo wa utambuzi wa NIDA una thamani ya Sh bilioni 161 na mkataba wa uendelezaji na utunzaji wa mfumo wa taarifa za ardhi ambao una thamani ya Sh bilioni 149.
Akizungumza wakati wa halfa hiyo ambayo ambayo pia ilishuhudiwa na Waziri Mkuu wa Korea Han Duck-Soo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania na Korea zinajivunia mahusiano yaliyodumu kwa miaka 30 ambayo yamekuwa chachu katika kukuza uchumi wa nchi hizo mbili katika sekta mbalimbali.
“Tunaishukuru sana Korea Kusini kwa kuwa miongoni mwa mataifa yanayoshiriki katika kutatua changamoto za kimaendeleo ikiwemo kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Korea (EDCF)”
Amesema kuwa kupitia mfuko huo, Tanzania imeweza kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo madaraja, barabara, kituo cha kisasa cha kusajili meli cha Zanzibar, njia ya kusafirishia umeme, hospitali ya Mloganzila, mradi wa umwagiliaji uliopo Zanzibar na utoaji huduma wa vitambilisho vya Taifa. “Miradi hii yote imegharimu zaidi ya dola za Kimarekani milioni 733.”