Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (Heslb) imetangaza nyongeza ya kozi mpya nne zitakazopewa kipaumbele katika utoaji wa mikopo kwa ngazi ya diploma kwa mwaka wa masomo 2023/2024.
Kozi hizo zitafanya kuwe na jumla ya kozi 10 kwa ngazi ya diploma zinazopewa kipaumbele katika utolewaji wa mikopo kwa ngazi hiyo ya elimu nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Heslb Disemba 26, 2023 kozi hizo ni pamoja na Uchimbaji madini na Sayansi ya Ardhi, Usafirishaji, Kilimo na Mifugo, pamoja na Uhandisi.
Itakumbukwa kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati akizindua utoaji wa mikopo kwa ngazi hiyo ya elimu nchini alisema kozi hizo za kipaumbele hupangwa kutokana na uhaba wa wataalamu katika kozi hizo.
“Tumenyumbulisha na kuanisha maeneo yenye uhitaji mkubwa zaidi ambayo mara nyingi Serikali ikitaka kuajiri watu haiwapati,” alisema Mkenda Octoba 6, 2023 jijini Dar es Salaam.
Wakati ukifurahia mapumziko ya Noeli, tunakuletea taarifa muhimu kuhusu stashahada zilizoongezwa ambazo wanafunzi wenye sifa watapangiwa mikopo.
Toleo la Pili la Mwongozo ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo ya Elimu kwa Wanafunzi wa Stashahada kwa 2023-2024’ linapatikana katika… pic.twitter.com/H2UBOAPsRV
— HESLB Tanzania (@HESLBTanzania) December 26, 2023
Dirisha la pili kufungwa Januari 4, 2024
Wakati Heslb ikitangaza kozi mpya za kipaumbele pia imebainisha kufunguliwa kwa dirisha la pili la maombi ya mkopo kwa ngazi ya diploma litakalofungwa Januari 4 mwakani.
Heslb imefafanua kuwa dirisha hilo linatawanufaisha makundi matatu ya wanufaika ikiwemo waliochelewa kuwasilisha maombi yao katika awamu iliyopita.
“Kundi la Kwanza ni wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Stashahada za kipaumbele kama zilivyotajwa katika ‘toleo la kwanza’ kwa mwaka 2023-2024’ ambao awali hawakuweza kuomba kwasababu mbalimbali ikiwemo kuchelewa hadi dirisha kufungwa,” imefafanua Heslb.
Kundi la pili ni wanafunzi wa mwaka wa pili au wa tatu wa Stashahada za kipaumbele kwa mwaka 2023-2024’ ambao hawakuweza kuomba mkopo awali. Kundi la Tatu ni wanafunzi wa Stashahada za kipaumbele zilizoongezwa kupitia mwongozo mpya uliotangazwa na Heslb.
Uamuzi wa Serikali kutoa mikopo kwa vyuo vya kati Tanzania ulitangazwa na wakati wa bajeti ya mwaka 2023/24 huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni mabadiliko sera ya elimu ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023.
Kutokana na uamuzi huo sasa vijana wa kitanzania waliokidhi vigezo wanaweza kupata mikopo itakayogharamia masomo hayo ya elimu ya juu na kulihakikishia Taifa uwezekano wa kuwa na wataalamu wa kutosha katika fani mbalimbali.