Rais Samia Suluhu Hassan, amepongezwa kwa kuleta suluhu nchini Tanzania kwa kuwaunganisha Watanzania bila kujali itikadi zao, dini au jinsia katika kuiongoza Tanzania.
Hayo yalisemwa na mwanamuziki Judith Wambura Mbibo maarufu kama Lady Jaydee wakati wa tamasha lake maalumu mwishoni mwa wiki la kumpongeza na kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake za kuijenga Tanzania mpya inayojali uhuru wa watu, demokrasia na usawa pamoja na haki za binadamu.
“Mimi na mwenzangu Rama D tumeandaa wimbo huu na kuzindua kampeni ya “nasimama na Mama Samia” katika kuleta suluhu Tanzania ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo bila kujali itikadi zao, imani zao na kuhakikisha kuna uhuru wa kweli na demokrasia nchini” alisema Lady Jaydee.
Akizungumza katika Tamasha hilo, Waziri wa habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akliisema Rais Samia Suluhu Hassan anaongozwa na mambo manne makuu katika kusimamia maendeleo ya nchi na Watanzania kwa ujumla ambayo ni MARIDHIANO, USTAHIMILIVU, MAGEUZI, KUJENGA UPYA TANZANIA (Reconsiliation, Resiliency, Reforms na Rebuilding The Nation.)
Akizungumzia Maridhiano Mheshimiwa Nape alisema Rais Samia anawaleta Watanzania pamoja bila kujali tofauti zao za kisiasa na kuhakikisha utawala wa sheria, usawa na kutobaguliwa, na fursa sawa kwa wananchi wote kujiendeleza kibinafsi, jamii na taifa kwa ujumla zinafanyika.
Pia alisema Rais katika utawala wake anahakikisha kuwa kila mtu anafurahia haki zake za msingi na kutekeleza majukumu yake kwa uhuru kwa mujibu wa sheria bila kubughudhiwa na chochote na kwa uhuru.
Akizungumzia nguzo ya pili ya Ustahimilivu Waziri Nape alisema Rais Samia anaamini katika ustahimilivu kwa kuhakikisha raia wote wa tanzania wanapatanishwa na wanapaswa kupona kutokana na shida yoyote iliyokuwepo huko nyuma katika awamu zote za uongozi wa nchi yetu na kusonga mbele katika kuijenga Tanzania ya kesho. Aliongeza kuwa watanzania wote wanapaswa kukabiliana na changamoto za maendeleo kama taifa katika umoja na mshikamano na kuhakikisha nchi inasonga mbele kwa kujiamini.