Lukuvi kutafuta suluhu na madalali

HomeKitaifa

Lukuvi kutafuta suluhu na madalali

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi anatarajia kukutana na madalali wa nyumba na viwanja jijini Dar es Salaam Desemba 13 mwaka huu baada ya kutoa kauli iliyoleta sintofahamu kuhusu ulipwaji wa madalali kodi ya mwezi mmoja pindi wawatafutiapo watu nyumba.

“Kumekuwa na tatizo la muda mrefu la madalali, serikali haina nia ya kufuta madalali kwa sababu wanatambulika na wanarahisisa kazi, lakini uchukuaji wa vipato vyao umekuwa na shida kutokana na kufanywa kwa kificho na baadhi yao wanafanya vibaya na ndio maana nimetoa tamko kwamba inafaa sasa aliyetuma kazi ndiye alipe,” alisema Lukuvi.

Pia Waziri Lukuvi aliweka wazi kwamba wanafahamu kuna baadhi ya madalali hawajasajiliwa na hawalipi kodi hivyo atazungumza nao ili waheshimike na serikali ipate kipato.

“Tunao ushahidi wanalipwa kotekote, mara zote lazima afiche siri nani mwenye nyumba , wameelewana nini, mwenye nyumba ana elewana na dalali lakini hana mamlaka yakuelewana na mpangaji. Sasa hii siri inawanufaisha madalali anachukua huku anachukua na huku, na tunaona ushahidi wa vielelezo kwa hili,” alisema Lukuvi.

Aliyazungumza hayo juzi jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kueleza mafanikio ya sekta ya ardhi katika miaka 60 ya Uhuru.

error: Content is protected !!