Mabasi mapya na ya kisasa 49 ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) yamewasili nchini yakiwa ya hadhi ya kimataifa.
Mabasi hayo ya Golden Dragon yaliyotengenezwa China, ni sehemu ya mabasi 99 ya mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita kuleta mageuzi ya usafiri wa mijini.
Tofauti na mabasi ya awali, yaliyowasili sasa yana mfumo wa kisasa wa viyoyozi na vitundu vya kuchajia simu katika kila kiti, teknolojia ambayo awali ilizoeleka kuonekana kwenye treni la Reli ya Kisasa (SGR), mabasi ya kisasa na kwenye ndege.
“Sasa, abiria wa Kimara, Korogwe, Mbezi, Morocco watasafiri kwa hadhi ya kimataifa huku mawasiliano yao yakibaki hewani wakati wote. Tunampa kongole ya dhati Rais Samia Suluhu Hassan,” ilieleza taarifa iliyotolewa na Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART).
Akipokea mabasi hayo bandarini jana, Mkurugenzi Mkuu wa UDART, Pius Ng’ingo alisema, “Dhamira ya Rais ni kumpatia mkazi wa Dar es Salaam huduma bora anayostahili. Mabasi haya 49 ni mwanzo tu, mengine 50 yanakuja hivi karibuni.
“Tuko katika hatua za mwisho za usajili na ukaguzi ili yaingie barabarani haraka iwezekanavyo.”


