Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema ameridhishwa na kasi ya utengenezwaji wa mabehewa mapya kwa ajili Reli ya Kisasa (SGR) ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) yanayotengenezwa na Kampuni ya Sung Shin Rolling Stock (SSRT) iliyoko Korea Kusini.
Majaliwa alisema hayo jana, baada ya kutembelea kampuni hiyo inayotengeneza mabehewa na injini za treni nchini Korea Kusini.
“Kati ya mabehewa 81 ambayo Tanzania inatengeneza kutola kwenu, tayari 36 yamekamilika yameshapelekwa nchini Tanzania na 45 yaliyobaki yanategemewa kukamilika Machi, 2023. Mabehewa haya ni ya daraja la tatu na yatatoa huduma zote muhimu,” alisema Waziri Majaliwa.
Majaliwa alimkaribisha rais wa kampuni hiyo, Gye Shul Park, kuja kuwekeza nchini kutokana na fursambalimbali zilizopo, ukiwemo mpango wa serikali wa kuendelea kuiboresha sekta ya usafiri wa reli.
“Mna kiwanda kikubwa, teknolojia ya hali ya juu pamoja utaalamu na wataalamu katika eneo hili. Kwa sasa tuna mipango mikubwa ya kuendelea kuiboresha sekta ya usafiri wa reli. Yapo maeneo tofauti katika mpango wa kuunganishwa na Reli ya Kisasa (SGR), nakukaribisha kuja kuwekeza kitu kama hiki Tanzania,” alisema Waziri Majaliwa.