Serikali yatangaza mgawo wa maji Dar na Pwani

HomeKitaifa

Serikali yatangaza mgawo wa maji Dar na Pwani

Serikali imetangaza mgawo wa maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani kwa sababu za kupungua kwa vyanzo vya maji vya Mto Ruvu Juu na Ruvu Chini.

Baada ya kutembelea vyanzo hivyo vya maji, Mkuu wa MKoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alisema taarifa aliyopewa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) ni kwamba vyanzo hivyo  vimeshuka uzalishaji maji kutoka lita milioni 466 kwa siku hadi lita milioni 300, sawa na asilimia 64.

Makalla alisema mgawo wa maji ni matokeo ya kiangazi kilichosababishwa na kukosekana kwa mvua za vuli, hivyo kusababisha kushuka kwa kina cha maji kwenye vyanzo hivyo.

“Kamati ya ulinzi na usalama mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro zilishatekeleza wajibu wa kudhibiti uchepukaji wa maji, hivyo asitokee yeyote akasema mvua zinaletwa na serikali au zinaletwa na sera ya Chama cha Mapinduzi, mvua ni kudra za Mwenyezi Mungu na hakuna makusudi yoyote kwamba maji yakosekane,” alisema Makalla.

Aidha, Makalla aliiagiza DAWASA iharakishe mradi wa visima vya maji Kigamboni utakaozalisha lita milioni 70 ili kupunguza adha ya maji kwa wakazi wa Kigamboni, Temeke na katikati ya jiji.

 

error: Content is protected !!