Mahakama ya Juu nchini Kenya imetupilia mbali ombi la Rais Mteule William Ruto la kupinga matumizi ya hati ya kiapo iliyowasilishwa na John Githongo, mwandishi wa zamani wa habari za uchunguzi nchini humo.
Githongo, katika hati yake ya kiapo, alidai Dennis Itumbi, mtaalamu wa mikakati ya kidijitali wa Ruto, alidukua tovuti ya IEBC.
Githongo aliwasilisha hati yake ya kiapo Jumatatu kuunga mkono ombi la urais la Raila Odinga ambapo anadai Itumbi alidukua tovuti na kubadilisha Fomu 34A ili kumpendelea Ruto.
“Fomu za Asili 34As zimefutwa na zile zilizopandishwa ni za takwimu za kughushi,” alisema Githongo. Itumbi ametupilia mbali madai hayo.
Ruto alitaka Mahakama ya Juu kufutilia mbali hati hizo za kiapo kwa msingi kuwa haziruhusiwi kwani zina taarifa za uvumi. Lakini Majaji wa Mahakama ya Juu walisema itakuwa mapema mno kuziondoa.
“Ni vyema mahakama iruhusiwe kuzingatia jumla ya ushahidi ulio mbele yake na kwa kuongozwa na kanuni za ushahidi iweze kutambua thamani na kizingiti cha ushahidi wa kila upande,” waliamua.
Ruto pia alikuwa ametaka vifungu fulani vya ombi la Raila vifutiliwe mbali lakini vivyo hivyo vilikataliwa kwa kukosa kushawishi mahakama.
SOURCE: HABARI LEO