Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia wakazi wanaohama kwa hiari yao kutoka katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuelekea kijiji cha Msomera, Handeni mkoani Tanga kuwa wataendelea na shughuli zao ikiwemo ufugaji katika mazingira bora zaidi.
Waziri Mkuu ambaye ameshuhudia wakazi hao takribani 127 kutoka katika kaya 27 wakihama na kuelekea kijiji cha Msomera, amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano katika kila eneo.
“Ninawaomba msafiri kwa amani kabisa na mioyo yenu ikunjuke. Isikilizeni Serikali yenu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Sasa hivi mko huru, nenda mkakae kwenye nchi yenu kwa uhuru,” amesisitiza leo Juni 23, 2022) wakati akiwaaga wakazi hao wanaohama kwa hiari yao kwenda kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo hilo.
Amesema uamuzi walioufanya wa kuhamia Msomera na kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo la Ngorongoro ni uamizi sahihi, hivyo ametumia fursa hiyo kuwahakikishia kwamba hakuna shughuli zao zozote zitakazisimama, wataendelea na ufugaji kwa kuwa Msomera kuna eneo kubwa na la kutosha.