Marekani yampongeza Rais Samia kwa uongozi bora

HomeKitaifa

Marekani yampongeza Rais Samia kwa uongozi bora

Huenda hatua ya kuboresha mifumo ya demokrasia nchini Tanzania iikaendelea kutoa matokeo chanya kutoka jumuiya za kimataifa mara baada ya Serikali ya Marekani kusema inafurahishwa na hatua hiyo na kuvutiwa kufanya uwekezaji.

Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris aliyekuwa akizungumza na wanahabari Ikulu jijini Dar es Salaam amesema yeye pamoja na Rais Joe Biden wanafurahishwa na jinsi Rais Samia Suluhu Hassan anavyoimarisha demokrasia na utawala bora nchini.

“Chini ya uongozi wako Tanzania imepiga hatua kubwa katika demokrasia, mimi na Rais Joe Biden tunajisikia fahari kwa hilo, umekubali kufanya kazi na vyama pinzani, umeondoa zuio la mikutano ya hadhara pamoja na kuimarisha uhuru wa kujieleza…, “ amesema Kamala.

Kamala ameongeza kuwa utawala bora huchochea uchumi stahimilivu na unaotabirika jambo ambalo huvutia uwekezaji hivyo Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania na kuwekeza katika nyanja mbalimbali za kiuchumi.

“Nina furaha kutangaza mipango mipya ya Serikali ya Marekani kwanza kupitia Benki ya Exim tutasaini mkataba wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 500 (Sh1.17 trilioni) za Tanzania ambapo zitasaidia uwekezaji katika masuala ya miundombinu, usafiri, teknolojia na na nishati safi, “ amesema Kamala.

Maeneo mengine ambayo Serikali ya Marekani inapanga kufanya uwekezaji ni pamoja na teknolojia ya intaneti yenye kasi ya 5G, usalama mtandaoni, pamoja na uwekezaji katika kiwanda cha kuchakata betri za magari ya umeme ambacho kinatarajiwa kukamilika mwaka 2026.

“Ubia huu utafanya kazi ya kutafuta fursa za ziada katika kanda kwa ajili ya kupata madini mengine muhimu ya kuchenjua katika kiwanda hicho kipya. LifeZone Metals itaanzisha kiwanda hicho mahali ambapo palikuwa na mgodi wa zamani wa dhahabu wa Barrick,” amesema Kamala.

error: Content is protected !!