Spika wa Bunge katika nchi yoyote ni kati ya viongozi wa juu, wanaoongoza mhimili muhimu sana katika nchi. Sio jambo la kawaida sana kusikia mtu anajiuzulu kutoka katika nafasi hiyo.
Barani Afrika wapo wengi waliowahi kujiuzulu katika nafasi hiyo, na hapa chini ni baadhi yao:
1. Abdula Gemeda – Ethiopia
Gemeda ambaye alikuwa anawakilisha jamii ya Oromo, alijiuzulu mwaka 2017 akidai kwamba serikali ya Ethiopia imekosa heshima kwa watu wa jamii yake hivyo haoni sababu ya kuendelea kuwa Spika wa Bunge hilo.
2. Kerea Ibrahim – Ethiopia
Kadhia iliyowapata Ethiopia mwaka 2017 ilijirudia tena mwaka 2020 baada ya mtu mwingine kusema hataki kuwa Spika wa Bunge. Nudugu Ibrahim Kerea alichukizwa na kitendo cha kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo.
3. Mohamed Sheikh Osman Jawari – Somalia
Alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Somalia mwaka 2012 lakini mwaka 2018 Wabunge wa Bunge hilo walipiga kura ya kukosa imani juu yake.
4. Guillaume Soro – Ivory Coast
Aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Taifa hilo la Magharibi mwa Afrika (2007 -2012). Alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la nchi hiyo mwaka 2012 na mwaka 2019 alijiuzulu ikitajwa kuwa sehemu ya mpango wake wa kusaka Urais wa nchi hiyo. Baadae alifunguliwa mashtaka na kutakiwa kwenda jela, alikuwa ameshakimbilia uhamishoni Ufaransa.
5. Job Ndugai – Tanzania
Amejiuzulu leo, Januari 6,2021 akisema kwamba ni uamuzi alioufikia kwa ajili ya maslahi mapana ya taifa, Serikali na chama chake (CCM).
Job Ndugai ambaye ni Mbunge wa Kongwa, amedumu katika nafasi hiyo tangu mwaka 2015.