Matinyi: Serikali haijaweka rehani kitu chochote

HomeKitaifa

Matinyi: Serikali haijaweka rehani kitu chochote

Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi amesema mkopo wa Sh 6.5 trilioni uliikopwa na Serikali nchini Korea utalipwa kwa kipindi cha miaka 40 kuanzia mwaka 2028.

Kauli ya matinyi inakuja ikiwa imepita siku moja tangu rais Samia Suluhu Hassan na Rais Yoon Suk Yeol wa Jamhuri ya Korea washuhudie utiaji saini wa mkopo huo huku kukiibuka taarifa mbalimbali za upotoshaji kuhusu mkopo katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.

Taarifa hizo zinadai kuwa Serikali ya Tanzania imeweka rehani baadhi ya rasilimali ikwemo sehemu ya bahari na madini ili kukidhi vigezo vya kupewa mkopo huo jambo ambalo Matinyi amesema kuwa si kweli.

“Serikali yetu haijaweka rehani kitu chochote wala mali yoyote kama ambavyo imelezwa na baadhi ya vyombo vya habari…mkopo huu hauna masharti yoyote ya kuweka rehani kitu chochote,” amesisitiza Matinyi wakati akizungumza na wanahabari Juni 4, 2024 jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wake mkopo huo kwa ajili ya miradi ya maendeleo una riba ya asilimia 0.01 ambayo inaufanya kuwa miongonni mwa mikopo nafuu ambayo Tanzania imewahi kukopa.

Msemaji huyo ameitaja mikopo mingine miwili ambayo nchi hiyo imewahi kuikopesha Tanzania ikiwemo wa Dola za Marekani milioni 733 (sawa na Sh1.9 trilioni) mwaka 2014 hadi 2020 na Dola za Marekani bilioni 1 (sawa na Sh2.6 trilioni) kati ya mwaka 2021 hadi 2025.

Ni ushirikiano wa kimkakati

Mtinyi amewaambia wanahabari kuwa ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili ulioanza tangu mwaka 2014 ni wa kimkakati katika maeneo mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo ambayo mingine tayari imeshafanyika.

Ameyataja maeneo hayo kuwa ni ujenzi wa Hospitali ya rufaa Mloganzila ambayo ni tawi la Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), awamu ya kwanza ya utoaji wa vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na utekelezaji wa mradi wa taka katika mkoa wa Iringa.

Miradi mingine ambayo ipo katika hatua ya utekelezaji ni pamoja na Ujenzi wa Bandari ya uvuvi Bagamoyo, ujenzi wa kituo cha mikutano ya kimataifa Zanzibar, Ujenzi wa chuo cha tehama mkoani Dodoma na mradi wa umwagiliaji visiwani Zanzibar.

error: Content is protected !!