Mdee: Watendaji wanaokiuka sheria wachukuliwe hatua

HomeKitaifa

Mdee: Watendaji wanaokiuka sheria wachukuliwe hatua

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeitaka Ofisi ya Rais –TAMISEMI kufanya uchunguzi na kuchukua hatua kwa watendaji watakaobainika wamekiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za utekelezaji wa miradi ya mendeleo .

Hayo yamebainishwa tarehe 24 Machi, 2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa Mhe. Halima Mdee (Mb) wakati wa majumuisho wa ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Halmashauri ya Wilaya ya Mtama na Manispaa ya Lindi, Mkoani Lindi.

“hii sio tu kwa Halmashauri hizi za Mkoa wa Lindi hapa nazungumzia Halmashuri zote nchini watendaji wanaokiuka kufuata Taratibu, Sheria na Kanuni za utekelezaji wa miradi wachukuliwe hatua”amesisitiza Mhe.Mdee

Mdee ameishauri Ofisi ya Rais –TAMISEMI kushughulikia suala la ongezeko la watumishi katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuwe na ufanisi na ubora wenye tija katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo hasa katika usimamizi wa miradi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Amesema suala la utoaji wa mikopo ya asilimia 10 watendaji wanatoa huduma hizo lakini pia hawafuati kanuni zilizopo kwenye utoaji wa mikopo kama inavyotakiwa na Serikali.

“Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati anatimiza miaka miwili alisema asilimia kubwa ya mikopo hii inayotolewa hua hairudi hivyo ni wajibu wa Wakurugenzi kusimamia mikopo”amesema Mhe. Mdee

Ameishauri Ofisi ya Rais- TAMISEMI kuongeza kigezo cha urejeshaji wa mikopo ya asilimia 10 ambapo Serikali iliweka dhamira njema ya kuwasaidia wananchi lakini inaonekana dhamira hiyo inatumiwa vibaya.

Aidha, Kamati imeishauri Ofisi ya Rais- TAMISEMI miongoni mwa vigezo vya kupima ustadi wa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kiongezwe kigezo cha ufanisi wa Mkurugenzi katika kutoa mikopo na kufuatilia ipasavyo marejesho ya mikopo hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa imewataka Wakurugenzi hao kutambua kuwa wameaminiwa na Rais Samia ili kumsaidia kwa kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu.

error: Content is protected !!