Waziri Ummy: Hakuna wagonjwa wapya wa Marburg

HomeKitaifa

Waziri Ummy: Hakuna wagonjwa wapya wa Marburg

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema hadi kufikia jana tarehe 25 Machi, 2023 hakuna wagonjwa wapya wa Marburg walioripotiwa licha ya kupokea tetesi sehemu mbalimbali mkoani hapa.

Hayo ameyasema jana alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari nakusema kuwa ugonjwa huo unaendelea kudhibitiwa.

“Tangu kuanza kwa ugonjwa huu hadi leo tumeendelea kuwa na jumla ya wagonjwa walewale Nane waliothibitika ambapo Watano kati yao walifariki na Watatu wanaendelea na matibabu katika vituo vya kutolea huduma vilivyoainishwa.” amesema Waziri Ummy

Aidha, waziri Ummy amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Wadau mbalimbali inaendelea kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huu kwa kutekeleza mikakati mbalimbali.

Waziri Ummy amesema miongoni mwa njia zilizotumika ni kuwaweka watu wote waliotangamana kwa namna mbalimbali na wagonjwa au wahisiwa, ambapo hadi jana jumla ya watu 205 wanaendelea kufuatiliwa kwa karibu.

“Watu hawa wote ni wanafamilia waliouguza wagonjwa na watumishi wa Afya waliohudumia wagonjwa wapo sehemu maalumu kwa siku 21 ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu kama watabainika na maambukizi.” amesema Waziri Ummy

error: Content is protected !!