Mfahamu Freeman Mbowe: CHADEMA, Benki Kuu, biashara, na kesi ya ugaidi

HomeMakala

Mfahamu Freeman Mbowe: CHADEMA, Benki Kuu, biashara, na kesi ya ugaidi

 Aikael Alfayo Mbowe, ni kati ya Watanzania waliojipatia umaarufu hata kabla ya uhuru wa Tanganyika. Mzaliwa huyo wa mkoa wa Kilimanjaro, alikuwa mfanyabiashara mwenye ushawishi mkubwa, na alikuwa miongoni mwa watu waliomuunga mkono Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere kwenye harakati za kudai Uhuru.
Mtoto wa 10 wa marehemu Mzee Aikael Mbowe, ni Freeman, aliyezaliwa Septemba 14,1961, kisha akabatizwa siku ya Uhuru wa Tanganyika yaani Desemba 9,1961.
Freeman Mbowe alisoma shule ya msingi Lambo mkoani Kilimanjaro, kabla ya kujiunga na shule ya sekondari Kolila mwaka 1976, na mwaka 1977 alihamia shule ya sekondari Kibaha aliposoma hadi kiadto cha tano. Aliendelea na kidato cha tano na cha sita katika shule ya Sekondari Ihungo mkoani Kagera.

Kazi Benki Kuu

Baada ya masomo ya sekondari na emafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa, Freeman Mbowe alipata kazi Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kama  ofisa wa benki katika Idara ya Fedha za Kigeni.

Mbowe alianza kazi hapo BOT April 1982, lakini wakati huo pia alikuwa anamsaidia Baba yake katika biashara zake ambazo zilikuwa jijini Dar es Salaam.

Mwaka 1986, Mbowe alikwenda kwa Gavana Msaidizi wa Benki Kuu (Bob Makani ambaye baadae alikuja kuwa mmoja wa waanzilishi wa CHADEMA) ili kuomba likizo bila malipo, akitoa sababu alikuwa anataka kwenda masomoni.

Ombi la Mbowe kupewa likizo bila malipo lilikataliwa na Bob Makani (Gavana Msaidizi wa wakati huo) ambaye alimuambia Mbowe asifike tena katika ofisi hiyo.

Huo ndio ulikuwa mwisho wa kazi ya Freeman Mbowe ndani ya Benki Kuu

Biashara

Pamoja na kushiriki katika biashara za Baba yake na biashara inayotajwa mara nyingi ya ukumbi wa starehe wa Billcanas jiji Dar es Salaam, Freeman Mbowe alianza kujikita katika biashara zake tangu mwaka 1985.

Mwaka 1985, Mbowe na rafiki yake Martin Omari walifungu kampuni ya FM Exports, iliyojihusiha na uvuvi na uuzaji wa samaki nje ya nchi. Walikuwa wanavua samaki hapa Tanzania na kuwapeleka katika mataifa kama Botswana, Omani na Hispania.

Pia Mbowe alikuwa akifanya biashara ya kusafirisha matunda kwenda nje ya nchi akitumia Shirika la Ndege la Gulf Air.

Tangu wakati huo hadi sasa Mbowe amefanya biashara nyingine nyingi ikiwemo kumiliki hoteli.

CHADEMA

Freeman Aikael Mbowe aliingia rasmi katika siasa mwaka 1992, na alikuwa miongoni mwa waasisi wa  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) chama ambacho kilisajiliwa usajili wa kudumu mwaka 1993 kwa namba 0000003.
Mbowe alikuwa miongoni mwa waasisi wa CHADEMA wenye umri mdogo, ambapo waasisi wengine ni pamoja na Edwini Mtei (Alikuwa Gavana wa Benki Kuu wakati Mbowe anafanya kazi huko) na aliyekuwa Gavana Msaidizi wa Benki Kuu Bob Makani (aliyemnyima Mbowe likizo bila malipo)
Mbowe aligombea Ubunge wa jimbo la Hai mwaka 1995 na kukosa, alifanikiwa kupata Ubunge katika jimbo hilo mwaka 2000.
Mbowe ndiye mgombea wa kwanza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CHADEMA. Kwenye chaguzi za mwaka 1995 na 2000 CHADEMA hawakusimamisha mgombea wa Urais hadi Mbowe alipogombania kiti hicho mwaka 2005 na kupata nafasi ya tatu nyuma ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete (CCM) na Profesa Haruna Lipumba (CUF).
Mbowe alirudi tena Bungeni mwaka 2010 baada ya kumshinda Godwin Kimbita wa CCM katika jimbo la Hai. Mwaka 2015 Mbowe alishindwa kwenye uchaguzi wa Ubunge.
Freeman Aikael Mbowe ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, nafasi aliyoitumikia tangu mwaka 2004.
Kesi ya ugaidi
Kwa sasa Freeman Aaikael Mbowe yuko mahabusu, kwani anakabiliwa na mashtaka ya ugaidi akiwa na wenzake watatu (Halfan Bwire, Adam Kasekwa na Mohammed Lingwenya)
error: Content is protected !!