Mikakati ya kuinusuru NHIF

HomeKitaifa

Mikakati ya kuinusuru NHIF

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali itachukua hatua mbalimbali ikiwemo kutibu mapema magonjwa yasiyoambukiza ili kuunusuru Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambao umeelemewa na mzigo wa madeni.

Amesema kuelemewa kwa NHIF kunasababishwa na magonjwa yasiyoambukiza, urasimu na kuingizwa kwa wasio watumishi wa umma ambao asilimia 99 ni wagonjwa.

Ummy aliyekuwa akizungumza na wanahabari jana Septemba Mosi 2022 jijini Dodoma amesema Serikali itaweka utaratibu wa kutambua na kutibu mapema magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la damu na kisukari na kuyatibu katika hatua za awali ili kupunguza gharama kubwa za matibabu.

“Tutaendelea kuimarisha afua za kushughulikia magonjwa yasiyo ya kuambukizwa katika hatua za awali ikiwemo kuyatambua mapema kabla hayajawa na athari kubwa,” amesema Waziri Ummy.

Suluhu nyingine ni kuongea idadi ya wanachama wa NHIF ili kuwezesha ukusanywaji wa mapato zaidi yatakayowezesha utoaji wa huduma kwa makundi ya wagonjwa wanaougua mara kwa mara.

“Kama tupo milioni 60 na asilimia 50 ni watoto, kwa hiyo tuna watoto milioni 20, Bima ikiwa ni lazima NHIF ikisajili watoto milioni 5 tu wataweza kuwahudumia watoto wagonjwa,” amesema Waziri Ummy.

Pia Waziri Ummy amesema wataongeza udhibiti wa vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya watoa huduma wanaolenga maslahi yao binafsi, sambamba na matumizi ya bima yasiyo na tija.

“Tumeona watu wanafika hospitali ya saratani Ocean Road, alafu kesho yake anahamishwa anapelekwa kwenye kliniki mtaani. Kuna uhuni hatutakubali mfumo huu utetereke tutasimama kwa kuchukua hatua,” amesema Ummy.

“Jingine ni wataalamu wetu, leo unaenda kituo cha afya cha Serikali, anakwambia kesho njoo kwenye kituo changu.”

Serikali inaangalia uwezekano wa kupunguza gharama za matibabu kwa baadhi ya huduma za afya ambazo ziliwekwa awali ili kuvutia hospitali nyingi kujiunga na mfuko huo kwa sababu hazikuwa na uhalisia.

Uwasilishaji wa malipo ya bima kwa wakati, hususani kwa wanachama wa hiari ambao kwa mujibu wa Ummy, wengi wao ndiyo hutumia asilimia kubwa ya mapato ya bima ikilinganishwa na watumiaji wa lazima wanaokatwa katika mishahara.

Bima ya afya kwa wote

Suluhu ya muda mrefu ya kuikoa NHIF ni kuanzisha sheria na bima ya afya kwa wote ambapo Waziri Ummy amesema mchakato wake uko katika hatua za mwisho.

Bima hiyo ikianza kutumika itafungamisha baadhi ya huduma muhimu ikiwemo usajili wa leseni na upatikanaji wa vitambulisho ili kuhakikisha kila mtu anaipata.

error: Content is protected !!