Nchi Uganda, Polisi wanachunguza tukio la madaktari kutoa figo kwa siri ya mjamzito Peragiya Muragijemana (20) mkazi wa Kijiji cha Lwemiggo, wilayani Mubende.
Mama huyo anaeleza kwamba alijifungua mikononi mwa kunga wa jadi lakini alishindwa kutoa kondo la nyuma na kusababisha kutokwa na damu nyingi.
“Nilipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mubende ambapo mume wangu, Amos Tiringanya alitakiwa kusaini hati ya kuniruhusu kufanyiwa upasuaji,” alisema Peragiya.
Mume wake alisema kuwa madaktari walimueleza kuwa njia pekee ya kuokoa maisha yake kwani alikuwa akivuja damu.
“Baada ya upasuaji, mke wangu alirudishwa wodini akiwa amepoteza fahamu na aliruhusiwa baada ya siku tatu kutokana na msongamano hospitalini. Tulimpeleka nyumbani kwa mama mkwe wangu,
“Lakini baada ya siku tatu, nilipigiwa simu na mama mkwe akinijulisha kuwa mke wangu amepata matatizo ya tumbo. Tulienda kwa uchunguzi wa juu ambao ulionyesha kuwa figo yake ya kulia haikuwepo. Nilitia saini tu hati inayokubali kuondolewa kwa uterasi ya mke wangu ili kuokoa maisha yake, si figo yake,” alisema Amos.
Msimamizi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mubende, Dkt. Onesmus Kibaya alishauri familia ya Muragijemana kuwa watulivu kwani hospitali hiyo inafanya uchunguzi huku na kueleza kwamba hospitali hiyo haina uwezo wa kufanya upasuaji wa figo.
“Mbali na hilo, hospitali ya Mubende haina uwezo wa kufanya upasuaji wa figo bali hufanywa katika hospitali ya Mulago,” alisema Dkt. Kibaya.