Mjue Bibi Titi Mohammed, Mwanamke aliyezishinda Marekani na Urusi

HomeKitaifa

Mjue Bibi Titi Mohammed, Mwanamke aliyezishinda Marekani na Urusi

Bibi Titi Mohammed, alizaliwa Dar es Salaam mwaka 1926, wazazi wake wote wakitokea Rufiji mkoa wa Pwani na walikuwa waumini wa dini ya Kiislamu. Baba yake Biti Titi alipinga kabisa binti yake asisome akihofia kuwa atabadilishwa dini kuwa Mkiristo kwani shule nyingi wakati huo zilikuwa chini ya makanisa.

Mama yake Bibi Titi hakupenda binti yake akose elimu hata ya msingi, mume wake alipofariki tu akamuandisha binti yake Shule ya Msingi. Bibi Titi alianza shule na huko ndipo akaanza kupata hamasa na muamko wa kupigania uhuru wa Tanganyika.

Alipomaliza elimu ya mkoloni, Bibi Titi aliolewa akiwa na umri wa miaka 14, lakini ndoa haikudumu ambapo aliachika baada ya kujifungua mtoto wake wa kwanza aitwaye Halima ambaye anaishi hadi hivi leo.

Bibi Titi alikuwa msanii mahiri sana, mwenye sauti nzuri inayoweza kuteka nyoyo. Kupitia kipawa chake hicho aliweza kuvuta watu wengi wenye shughuli mbalimbali ambazo alihusika kuimba.

Mwaka 1950 Bibi Titi alianza harakati rasmi za kupigania Uhuru, alikutana na Nyerere kwa mara ya kwanza 1954 baada ya Chama cha TANU kuundwa. Bibi Titi na Nyerere wakawa marafiki wa karibu na harakati zikaendelea. Bibi Titi akahusika kuunda Umoja wa Wanawake Tanzania na kuwa Mwenyekiti 1955, ndani ya miezi mitatu tu aliweza kusajili wanawake 5000 kwenye chama.

Kati ya mwaka 1960 – 1970 Bibi Titi alizuru taifa la China mara tatu kama safari binafsi na kazi za Serikali akiwakilisha Chama cha TANU. Serikali ya China ilitambua bayana mchango wa wanawake katika harakati za kupigania uhuru na kupigana na ubepari, hivyo ushawishi wa Bibi Titi kwenye kukusanya watu kwa hotuba na matendo yake, vilivutia sana Serikali ya China hadi kumualika mara kadhaa kuzungumza nae.

Ikumbukwe wakati huo Dunia ilikuwa kwenye vita Baridi kati ya Marekani pamoja na Umoja wa nchi za kisovieti, lakini Bibi Titi alikuwa ni mjuvi sana katika diplomasia katika kulinganisha mahusiano kati ya Urusi na Marekani na kwa maslahi ya Tanzania. Aliwahi kuhudhuria kote Moscow Urusi hadi White House Ikulu ya Marekani ambapo alikutana na wawakilishi wa Taifa la Taiwan, China na mataifa mengine kwa maslahi ya Tanzania.

Mwaka 1963 kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, China ilialika wanawake kutoka Tanganyika, Zanzibar pamoja na Kenya. Lengo wanawake hao kualikwa ilikuwa ni kwenda kujifunza stadi za ushonaji na pamoja na misingi ya siasa za kijamaa katika kuendesha uchumi na kupigana na uchumi wa kibepari. Wakati wa ziara hiyo Beijing China, Bibi Titi alipata wasaa wa kufikisha ujumbe wake kutoka Serikali ya Chama cha TANU, alisema “Umoja w Wanawake Tanzania (UWT) unajenga jengo jipya Dar es Salaam litakalokuwa na vyumba vikubwa kati ya saba au nane, na kila chumba kinahodhi kati ya watu 30 hadi 40, lengo letu ni kuanzisha sehemu ya mafunzo ya ushonaji kwa kina mama ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuondoa utegemezi kutoka kwa mabepari.”

Hotuba yake hiyo ilipendwa sana na Chama cha Serikali ya China hadi kuahidi kuchangia vyerehani katika jengo hilo na utekelezaji wa shughuli hiyo ianze mara moja pindi Bibi Titi atakaporejea Tanganyika. Bibi Titi alitumia vyema kipawa chake cha Diplomasia katika kuhakikisha Tanganyika inashinda maslahi vizuri, mfano, wakati mmoja aliwahi kuishawishi Serikali ya Marekani kuchangia ujenzi wa vituo vya kulelea watoto, Serikali ya Marekani ilikubali na kutoa mchango huo, na wakati huo ikumbukwe kuwa Tanganyika ilikuwa rafiki wa karibu wa Urusi pamoja na China.

Baada ya azimio la Arusha 1967, Bibi Titi aliingia mgogoro na Mwalimu baada ya kupinga wazi baadhi ya sera za Ujamaa, 1969 Bibi Titi alishitakiwa na kesi ya uhaini na kesi yake iliendeshwa kwa siku 127. Bibi Titi alikutwa na hatia na kufungwa kifungo cha maisha jela na kuwa Mtanzania wa kwanza kuhumiwa kwa kesi ya uhaini akiwa na wenzake sita.

Akiwa Gerezani mume wake wa pili alimtaliki, na mwaka 1972 alitoka kwa msahama wa Rais Nyerere. Baada ya kutoka gerezani maisha yake kwa wingi aliishi nchini Afrika ya Kusini, alfariki huko huko mwaka 2000 wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Net Care Johannesburg.

Huyo ndiyo Bibi Titi, mpigania Uhuru wa nchi yetu Tanzania.

error: Content is protected !!