Wakati zoezi la kuweka vibao vya majina ya mitaa nchini likiendelea, mchekeshaji kutoka kundi la Mizengwe, Hemedi Khalidi Maliaga maarufu kama Mkwere amepata heshima baada ya wananchi kukubaliana jina la msanii huyo kuwekwa kwenye kibao cha mtaa wao.
Akishiriki katika uwekwaji wa kibao kilichoandikwa Mtaa wa Mkwere, Mkwere alisema anashukuru sana uongozi na wananchi wote waliokubali kutumia jina lake huku akiahidi kuhakikisha mtaa huo unalindwa na kutambulika kwa sifa nzuri.
“Nawashukuru sana kwa sababu mimi hii kwangu imekua kama- surprise, kuweza kupewa mtaa kwa kutumia jina langu kiukweli nawashukuru sana viongozi wangu, komredi Henry Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Rais Samia na Mkurugenzi wa manispaa, kiukweli nimefurahi sana siku ya leo kuweza kupewa heshima,” alisema Mkwere.
Naye Diwani wa kata ya Kimara, Ismail Mvungi amesema zoezi la uwekaji wa vibao vya barabara za mitaa zimeanza rasmi na ameshukuru wananchi wote walioshiriki katika zoezi hilo huku akisema sasa limeanza rasmi Kimara nzima.