Mnada wa zao la chai nchini unaotarajiwa kuanza kufanywa jijini Dar es Salaam mwaka huu, huku serikali ikitangaza neema kwa wakulima kwamba hautakuwa na tozo.
Akifungua mkutano wa wadau wa zao la chai nchini uliofanyika mjini Iringa jana, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema uanzishwaji wa mnada huo ambao hatua zake zimekamilika, unakwenda sambamba na uanzishwaji wa maabara, maghala ya kuhifadhi zao hilo pamoja na ujenzi wa mazingira mazuri ya biashara ya majani ya chai.
“Mnada hautakuwa na tozo kwani serikali imekubali pia kuzibeba tozo hizo kwa manufaa ya taifa na wazalishaji wa zao hilo,” alisema bila kuzitaja tozo hizo.
Alisema kuanzishwa kwa mnada huo kutaongeza tija na ufanisi kwenye sekta ya chai utakaokuwa na manufaa na faida nyingi kwa wakulima wa zao hilo nchini.
Akitoa mfano alisema mnada huo utapunguza gharama za usafirishaji, utawezesha kutawala bei yake sokoni, kuongeza uwazi na uhakika wa ubora wa madaraja ya chai.