Moshi mweupe mradi wa LNG

HomeKitaifa

Moshi mweupe mradi wa LNG

Waziri wa Nishati, January Makamba, ametembelea ofisi za Kampuni ya Shell, nchini Uholanzi, na kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa kampuni hiyo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na utekelezaji wa mradi wa LNG nchini. 

Katika mazungumzo hayo na Bwana Cederic Cremers, Makamu wa Rais anayeshughulikia miradi ya LNG na Bwana John Crocker, Makamu Rais wa Shell anayehusika na Mahusiano ya Serikali, Waziri Makamba alielezea azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha mazungumzo yanakamilika mwezi Disemba mwaka huu na hatua za utekelezaji zinaanza mara baada ya hapo. 

Katika mikutano hiyo, Waziri Makamba pia alielezea mpango wa Serikali wa kuanzisha Ofisi Maalum ya Kusimamia Utekelezaji wa Mradi wa LNG (Tanzania LNG Office) mnamo mwezi Novemba mwaka huu kwa lengo la kuratibu, kuharakisha na kurahisisha hatua za utekelezaji wa mradi. 

Mradi huo wa kuchakata na kusindika gesi asilia iliyogundulika katika bahari kuu Kusini mwa Tanzania, utaleta nchini uwekezaji wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 40, unatekelezwa na Makampuni ya Shell ya Uholanzi na Equinor ya Norway na washirika wao. 

error: Content is protected !!