Mradi mkubwa Tanzania

HomeKitaifa

Mradi mkubwa Tanzania

Tatizo la uhaba wa maji huenda likawa historia katika miji 28 nchini Tanzania ukiwemo Muheza mkoani Tanga  pale utakapokamilika mradi wa maji katika miji hiyo wenye thamani ya Sh1.2 trilioni.

Mradi huo ni matokeo ya ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali ya Tanzania na India ambapo India kupitia benki ya Exim imeikopesha Tanzania kiasi hicho cha fedha ambacho kitatumika kujenga mindombinu ya maji na kusambazwa kwa wananchi wa maeneo hayo.

Kati ya fedha hizo zilizotolewa na India,  Tanzania bara imepata Dola za Marekani milioni 465 (Sh1.1 trilioni) na kiasi kilichobaki kitapelekwa Zanzibar.

Miji iliyobahatika kupata neema hiyo ni Muheza, Handeni na Pangani mkoani Tanga, Makonde, Nanyumbu  na Kilwa Masoko (Mtwara), Ifakara (Morogoro), Chunya na Rujewa (Mbeya) na Songea mkoani Ruvuma.

Miji mingine ni Njombe, Wanging’ombe na Makambako mkoani Njombe, Mafinga (Iringa), Mpanda (Katavi), Sikonge, Urambo na Kaliua (Tabora),  Singida, Kihomboi na Manyoni (Singida), Chemba na Chamwino (Dodoma), Kasulu (Kigoma), Kayanga (Kagera) ,Geita na Chato (Geita), Rorya, Mugumu na Tarime (Mara).

Ikiwa mradi huo utatekelezwa kikamilifu utakuwa ndiyo mradi mkubwa zaidi Tanzania kuzidi miradi ya miradi ya Tabora- Igunga-Nzega uliojengwa kwa Sh617 bilioni na mradi wa Arusha wenye thamani ya Sh520 bilioni.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyeshudia utiaji saini wa mradi huo leo Mei 6, 2022 jijini Dodoma ameishukuru India kwa ushirikiano wake mzuri na sapoti inayoendelea kutoa kwa Serikali ya Tanzania katika masuala ya biashara na elimu.

Pia ameipongeza Wizara ya Maji kwa kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji jambo lililosaidia mradi huo kunufaisha miji 28 tofauti na miji 16 tu iliyokuwa imekadiliwa awali.

Pamoja na pongezi hizo Rais Samia amewataka watendaji wa Wizara ya Maji kusimamia ipasavyo ujenzi wa mradi huo ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miundombinu inajengwa ipasavyo na maji yanapatikana kwani mradi huo unajengwa kwa fedha za mkopo na unatakiwa kulipwa.

“Nendeni mkasimamie fedha zetu huu ni mkopo, kwa mara nyingine tumekuja mbele ya wananchi kuwaeleza tumepata mkopo wa dola milioni 500 na zote zinakwenda kwenye majivkwenye miji iliyotajwa.

“Na kwa sababu ni mkopo, Watanzania wote tutakuja kuulipa mkopo huu kwa hiyo nendeni kasimamieni mkopo ulete manufaa wanapokuja kuulipa wawe wanatumia matunda ya mkopo waliochukua,” amesema Rais.

 

 

 

 

 

 

 

error: Content is protected !!