Huenda wakazi wanaoishi kusini mwa jiji la Mwanza wakaondokana na shida ya upatikanaji wa maji safi na salama baada ya Serikali kuweka mikakati ya kuboresha huduma hiyo.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwausa) imesaini mkataba wa Euro milioni 2 sawa na Sh4.7 bilioni na kampuni ya Seureca Consulting Engineering ya Ufaransa wa kujenga miradi ya maji katika Mkoa wa Mwanza.
Seureca itashirikiana na kampuni ya Netwas ya Tanzania kufanya upembuzi yakinifu, usanifu na usimamizi wa ujenzi wa mradi wa miundombinu ya kupeleka maji maeneo ya kusini mwa Jiji la Mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwauwasa, Mhandisi Leonard Msenyele aliyekuwa akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo juzi Julai 19 jijini Mwanza, amesema mkataba huo ni hatua za awali za utekelezaji wa mradi wa kufikisha huduma ya maji kwenye maeneo ya Wilaya za Nyamagana, Misungwi na Magu.
Maeneo yatakayonufaika na mradi huo ni Buhongwa, Nyamazobe, Sahwa, Lwanhima, Fumagila, na Kishiri wakati kwa upande wa Wilaya ya Misungwi maeneo ya Usagara, Nyashishi, Nyang’homango, Kigogo Ferry, Bujingwa.
Kwa upande wa Wilaya ya Magu ni Kisesa, Bujora, Isangijo, Kanyama, Igekemaja na Ihayabuyaga.
Mkataba huo umegawanyika katika sehemu mbili ya kwanza ikiwa ni kufanya upembuzi yakinifu, tathmini ya athari za mazingira na kijamii na usanifu na sehemu ya pili ni kumsimamia mkandarasi atakayetekeleza mradi huo.
Uhitaji wa huduma ya maji kwenye maeneo hayo ni mkubwa na kwamba wananchi wa maeneo hayo wanayo matarajio makubwa na mradi huo hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya maeneo hadi hivi sasa hayana mtandao wa maji safi.
“Kuna uhitaji mkubwa wa huduma ya maji kwenye maeneo haya; ni matumaini yangu kwamba kutokana na uzoefu wenu mtafanya kazi kwa mujibu wa mkataba, wananchi wanahitaji maji, hawataki kutusikia tukizungumzia habari za michakato” amesisitiza Mhandisi Msenyele.
Amezihakikishia kuzipa ushirikiano wa karibu kampuni hizo na amezielekeza kuanza shughuli zake mara moja ili mapema mwaka 2023 shughuli za ujenzi wa mradi zianze.
Shughuli hizo zitahusisha ujenzi wa vituo vinne vya kusukuma maji, ujenzi wa matenki manne ya ujazo tofauti ya kuhifadhia maji, uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa mabomba za kusambazia maji yenye urefu wa takriban kilomita 400.
Mhandisi Mshauri wa Seureca Afrika Mashariki, Christophe Lacarin aliihakikishia Serikali kuwa watakamilisha shughuli za mradi kwa wakati na kwa ubora mkubwa kulingana na uzoefu wa muda mrefu walionao kwenye shughuli za usanifu na usimamizi wa miradi.
“Tunauhitaji huu mradi, tunaimani kwa ubora wa kazi zetu mradi huu utatuletea miradi mingine mingi na tumetekeleza miradi mingi maeneo mbalimbali duniani ambayo inaendelea kututengenezea mazingira ya kupata kazi,” amesema Lacarin.
Mkataba huo ni wa miezi 44 na utekelezaji wake unapaswa kuanza ndani ya siku 28 kutoka siku ya utiaji saini.